UPANDAJI MITI MALISHO
*Hatua za Kuanzisha Shamba la Miti Malisho*
• Kuchagua eneo lenye rutuba lilimwe kabla ya mvua kunyesha
• Kuandaa mbegu na kuanzisha kitalu cha miti miezi mitatu kabla ya msimu wa mvua
• Kupanda mbegu au tumia vipando kutoka miti iliyokomaa au miche kutoka kitaluni kwa vipimo mita 1 kwa mita 1 kutoka mche hadi mche na mstari hadi mstari
• Kuzungushia wigo pembeni ili kuzuia wanyama wasipite na kuharibu miti
• Kupalilia mara kwa mara ili kuondoa magugu na kuzuia moto
_Tambua kuwa Kilo 1 ya mbegu zinaweza kutumika kupanda shamba la ekari moja_
*Jinsi ya Kuvuna Miti Malisho*
• Kutunza miti kwa miaka miwili na kuanza kuikata sm 50 kutoka ardhini ili kupata machipukizi mengi na meroro kwa ajili ya kulisha mifugo
• Uvunaji wa majani ya miti malisho waweza kufanyika kila yanapochipua kwa kipindi chote cha mwaka.
• Ni vizuri kukata machipukizi kabla hayajakomaa, kata machipukizi yanapokuwa na urefu wa mita moja hivi.
• Fahamu kuwa kadiri machipukizi yanavyokomaa ndivyo viinilishe vinavyopungua.
*Namna ya Kuandaa Miti Malisho kwa Ajili ya Kulisha Mifugo*
• kukata majani ya kutosha toka shamba la malisho
• Kuyaanika kivulini kwa muda wa siku mbili
• Kuyafikicha na kutoa vijitawi
• Kutayarisha pumba na madini (chumvi)
• Kuchanganya majani hayo pamoja na pumba na madini (chumvi) kwa kipimo cha kilo moja ya pumba kwa kilo mbili za majani yaliyokaushwa kwa ajili ya kulisha mifugo hasa ng’ombe wanaokamuliwa hutumika kama mbadala wa kutumia mashudu ya pamba au alizeti ambayo ni ghali sana.
• Lakini pia miti malisho yaweza kulishwa moja kwa moja kwa mnyama au kukaushwa kama ‘leaf meal’
• Kumpatia ng’ombe kiasi cha kilo 2 - 3 kwa siku hasa wakati wa kukamua.
*Jinsi ya Kuhifadhi Malisho ya Ziada*
• Kata majani (machipukizi) kabla ya kukomaa.
• Kuyaanika kivulini kwa muda wa siku mbili au tatu kisha kuyafikicha na kutoa vijitawi.
• Kuweka majani katika magunia au mapipa na kuyahifadhi mahali pasipo na unyevu tayari kwa kulisha mifugo yako wakati wa kiangazi.
Miti malisho inaweza kupandwa kwenye mipaka ya shamba au ndani ya shamba, eneo la kuzunguka nyumba kama uzio, maeneo maalumu kama vishamba vidogo vidogo, katika miinuko shambani na kwenye matuta ya kuzuia mmomonyoko wa udongo.