Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA, KILIMO NA MIFUGO
09 Aug, 2024
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA, KILIMO NA MIFUGO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deodatus Philip Mwanyika imeitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuendelea kusambaza teknolojia bora za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo kwa wafugaji.

Kamati hiyo imetoa agizo hilo leo tarehe 07/08/2024 ilipotembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya 31 ya Kilimo ya Kimataifa (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika ndani ya viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’

Sambamba na hayo kamati hiyo imeipongeza TALIRI kwa jinsi ilivyojipanga kutoa elimu katika maonesho hayo juu ya teknolojia bora za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo ikiwemo mbari bora za mifugo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na mazao mengine ya mifugo pamoja na elimu ya mbegu bora za malisho na vyakula vya mifugo.

Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Janejelly Ntate James amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni ya TUTUNZANE MVOMERO ikiwa na maana ya mkulima kumtunza mfugaji na mfugaji kumtunza mkulima ili kuondoa migogoro baina ya wafugaji na wakulima.

“TALIRI mna jukumu la kuhakikisha kampeni hiyo inatekelezeka kwa kuhamasisha wafugaji kuacha kufanya ufugaji wa kuhama hama ili kuepuka mifugo yao kuingia kwenye maeneo ya watumiaji wengine wa ardhi hivyo ni wakati sasa wa kuwa na mkakati madhubuti wa kusambaza elimu ya malisho bora ya mifugo kwa wafugaji” ameeleza Mhe. Janejelly.

Kwa upande wa Meneja wa Sehemu ya Uhaulishaji wa Teknolojia wa TALIRI Ndg. Gilbert Msuta ameeleza kuwa TALIRI imeendelea kuhakikisha wafugaji wanapata elimu stahiki ya teknolojia bora za mifugo ambapo taasisi hiyo imekuwa ikitembea wafugaji lakini pia wafugaji wamekuwa wakitembelea vituo mbalimbali vya taasisi hiyo vinavyopatikana kwenye kanda zote nchini ili kupata elimu ya ufugaji wenye tija.