KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA TALIRI KWA UZALISHAJI WA MALISHO

Kamati ya kudumu ya Bunge ya viwanda, Biashara, Mifugo na Kilimo imeipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa kazi nzuri ya kuzalisha na kusambaza malisho bora ya mifugo nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 18/03/2025 katika ziara ya kamati hiyo ya kutembelea kituo cha TALIRI Mpwapwa kwa lengo la kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia malisho wenye thamani ya shilingi Milioni 219, ghala hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi marobota 30,000 kwa wakati mmoja tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo maghala yaliyopo yalikuwa na uwezo wa kuhifadhi marobota 14,000 pekee.
Akiongea Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb) amesema kamati imeridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Wizara kupitia TALIRI juu ya jitihada za uzalishaji wa malisho bora na kwamba utekelezaji wa mradi huo utaongeza tija kwenye ufugaji kutokana na upatikanaji wa malisho.
“Tunawapongeza kwa usimamizi wa mradi huu uliozingatia thamani ya fedha na tunaamini uzalishaji wa malisho na mbegu zake utaongezeka ili kuwezesha wafugaji nchini kufuga kwa tija” Alisema Mhe. Mwanyika.
Kwa upande wake Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) Waziri wa Mifugo na Uvuvi ameihaidi kamati hiyo kuendelea kusimamia fedha zote za miradi zinazoidhinishwa kwa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, Dkt. Kijaji amemshukuru Mhe. Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuboresha sekta za uzalishaji ikiwemo Mifugo kwa kuwezesha kupatikana kwa malisho bora ya mifugo na hivyo kuwezesha ufugaji wa kibiashara.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Erick Komba amesema kuwa ujenzi wa ghala hili utawezesha kituo cha TALIRI Mpwapwa mbali na kuongeza uwezo wa kuhifadhi malisho pia utawezesha upatikanaji wa malisho kwa mwaka mzima, kulinda ubora wa malisho pamoja na kupunguza upotevu wa malisho kutokana na kukosekana kwa mahali pa kuhifadhia malisho hasa kipindi cha masika.