Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MAENEO YA MALISHO YAFIKIA HEKTA MILIONI 3.69 NCHNI
18 May, 2026
MAENEO YA MALISHO YAFIKIA HEKTA MILIONI 3.69 NCHNI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za malisho nchini kupitia upangaji bora wa matumizi ya ardhi, hatua iliyowezesha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kufikia hekta milioni 3.69 mwaka 2025/2026.

Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji mbalimbali nchini.

Akizungumza leo Mei 14, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2025/2026 ya Wizara hiyo katika kikao cha 29 cha mkutano wa tatu wa Bunge la 13 kilichofanyika katika ukumbi wa Ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, Mheshimiwa Bashiru amesema kuwa katika mwaka 2025/2026 pekee jumla ya hekta 196,324.25 za maeneo ya malisho zimetengwa kupitia mipango hiyo.

Taarifa hiyo iliwasilishwa ikiwa ni sehemu ya mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mhe. Bashiru ameendelea kueleza kuwa shughuli hiyo imefanyika katika vijiji 187 vya wilaya 22 zilizopo katika mikoa 18 nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa maeneo rasmi ya malisho na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi.

“Hatua hizi zimewezesha kuongeza maeneo ya malisho kutoka hekta milioni 3.49 mwaka 2024/2025 hadi kufikia hekta milioni 3.69 mwaka 2025/2026,” amesema.

Aidha, Waziri huyo amesema hadi kufikia Aprili 2026, jumla ya hekta milioni 1.35 katika vijiji 365 zimepimwa na kutangazwa rasmi, huku hekta 216,971.56 katika vijiji 114 zikifanyiwa upembuzi na uhakiki kwa ajili ya kutangazwa katika Gazeti la Serikali.

Serikali imeendelea kusisitiza uwekezaji katika uzalishaji na uhifadhi wa malisho bora kama sehemu ya mkakati wa kuongeza tija, kuimarisha uzalishaji wa mifugo na kukuza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.