WAFUGAJI MUHEZA WAJIFUNZA MBINU BORA ZA UFUGAJI WA NG'OMBE WA MAZIWA MUFINDI
Ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya mafunzo, wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka wilayani Muheza mkoani Tanga wanaonufaika na Mradi wa Maziwa Faida, tarehe 20/02/2026 wametembelea wafugaji wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa kwa lengo la kujifunza mbinu bora na za kisasa za kuboresha uzalishaji wa maziwa. Ziara hiyo imelenga kuwajengea uwezo wafugaji katika nyanja ya lishe, afya ya mifugo na uongezaji thamani wa maziwa.
Ziara hiyo imewezeshwa na Mradi wa Maziwa Faida unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland Tanzania na kutekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki kwa kushirikiana na Taasisi ya Mamlaka ya Chakula Ireland (Teagasc), ukilenga kuboresha mnyororo wa thamani wa ng’ombe wa maziwa nchini.
Katika mafunzo hayo, wafugaji walitembelea shamba la mfugaji anayezalisha malisho aina ya Juncao, Cenchrus ciliaris na Rhodes na kujifunza namna bora ya kuotesha, kuzalisha mbegu, kuvuna na kuhifadhi malisho hayo yenye tija katika kuongeza uzalishaji na ubora wa maziwa.
Aidha, walipata fursa ya kujifunza teknolojia ya kuogeshea mifugo kwa mfumo wa ‘spray race’ unaosaidia kudhibiti kupe na magonjwa ya ngozi kwa ufanisi, pamoja na mbinu sahihi za kuchakata na kuhifadhi nyasi kwa ajili ya chakula cha mifugo hasa kipindi cha ukame.
Wafugaji hao pia walitembelea kituo cha kukusanyia na kuchakata maziwa kinachozalisha mtindi, yoghurt na maziwa fresh, hatua inayoongeza thamani ya maziwa na kupanua fursa za masoko kwa wafugaji wadogo na wa kati.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku ambae pia ni Msimamizi Mkuu wa mradi huo aliwahimiza wafugaji kuyatumia mafunzo hayo kama chachu ya kuongeza maarifa, kuboresha uzalishaji na kuongeza kipato, huku wakichangia ukuaji wa sekta ya maziwa nchini.
Kwa niaba ya wafugaji wenzake, Bi. Lightness Mbwana alishukuru kwa mafunzo hayo akisema yataongeza tija na kuleta mabadiliko chanya katika shughuli zao za ufugaji.
