Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
HEKTA ZAIDI YA LAKI 7 ZA MALISHO ZATENGWA NDANI YA MIAKA 4 YA SERIKALI.
12 May, 2025
HEKTA ZAIDI YA LAKI 7 ZA MALISHO ZATENGWA NDANI YA MIAKA 4 YA SERIKALI.

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga hekta 700,799.96 za malisho nchini lengo ikiwa ni kumpunguzia mfugaji mzigo wa kuzunguka na mifugo nchi mzima kutafuta malisho.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) wakati akiongea na wanahabari jijini Dodoma kwa ajili ya kuelezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Waziri Kijaji ameendelea kueleza kuwa idadi hiyo imeongeza maeneo ya malisho kutoka hekta 2,788,901.17 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia hekta 3,489,701.13 mwaka 2024/2025 na amewataka wafugaji kuhakikisha wanapanda malisho kwa ajili ya mifugo yao ili kuondoa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Aidha, Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa katika mwaka 2024/2025 Wizara imekamilisha ujenzi wa ghala katika shamba la malisho lililopo kituo cha TALIRI Mpwapwa kwa ajili ya kuhifadhia malisho na mbegu za malisho huku ujenzi wa maghala mengine ukiendelea katika shamba la malisho la Vikuge (Kibaha) na Langwira (Mbalari)

Pamoja na hayo Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa Wizara imefanikiwa kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa vyakula vya mifugo na kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa vyakula vya mifugo vilivyosindikwa kutoka tani 1,380,000 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia tani 2,600,000 kwa mwaka 2024/2025.

Akiongelea mwenendo wa bajeti ya Wizara hiyo Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa bajeti imeendelea kuongezeka kutoka shilingi 169,194,996,999 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi 460,333,602,000 kwa mwaka 2024/2025 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 172.07. Hii ina maana kuwa katika kipindi hiki, Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza uwekezaji na tija katika huduma za mifugo na uvuvi kwa zaidi ya asilimia 100.

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ikiwa ni moja kati ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo inajivunia kwa mafanikio hayo na mengineyo makubwa ambayo yameongeza tija kwa shughuli za ufugaji nchini.