Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
ZAIDI YA WAFUGAJI 3,000 MUHEZA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UFUGAJI BORA KUPITIA MRADI WA MAZIWA FAIDA
13 May, 2026
ZAIDI YA WAFUGAJI 3,000 MUHEZA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UFUGAJI BORA KUPITIA MRADI WA MAZIWA FAIDA

ZAIDI YA WAFUGAJI 3,000 MUHEZA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UFUGAJI BORA KUPITIA MRADI WA MAZIWA FAIDA

Mradi wa Maziwa Faida unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti, Ushauri na Mafunzo ya Kilimo na Chakula nchini Ireland (Teagasc) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, umefanikiwa kutoa mafunzo ya ufugaji bora kwa zaidi ya wafugaji 3,000 kutoka Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene, wakati wa mahojiano na mwanahabari yaliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za LITA Buhuri jijini Tanga.

Dkt. Mwambene amesema kupitia utekelezaji wa mradi huo, LITA imeendelea kuwawezesha wafugaji kwa kuwapatia maarifa na mbinu bora za ufugaji wa kisasa zinazolenga kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuboresha afya ya mifugo pamoja na kuongeza kipato cha wafugaji.

Amefafanua kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, LITA ina jukumu la kutoa mafunzo kwa mfumo unaojumuisha asilimia 40 ya nadharia na asilimia 60 ya vitendo ili kuhakikisha wafugaji wanapata uelewa wa kina pamoja na uzoefu wa moja kwa moja katika shughuli za ufugaji bora.

“Mafunzo haya yanatolewa kupitia ziara za ugani zinazofanyika katika maeneo ya wafugaji pamoja na ziara za mafunzo zinazowezesha wafugaji kutembelea LITA Buhuri kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo kuhusu teknolojia mbalimbali za kisasa za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa,” amesema Dkt. Mwambene.

Aidha, amesema mradi huo umeendelea kuwa chachu ya mabadiliko kwa wafugaji wengi kwa kuwawezesha kutumia mbinu bora za lishe, uzalishaji wa malisho, usimamizi wa afya ya mifugo pamoja na matumizi ya teknolojia rafiki zinazochangia kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa.