Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MRADI WA MAZIWA FAIDA WAWAVUTIA WAFUGAJI
01 Apr, 2025
MRADI WA MAZIWA FAIDA WAWAVUTIA WAFUGAJI

Wafugaji wa Wilaya ya Muheza wanaonufaika na Mradi wa Maziwa Faida wameomba mradi huo uendelee kutekelezwa ili kuweza kunufaisha wafugaji wengi zaidi nchini.

Wafugaji hao wametoa ombi hilo leo tarehe 15/03/2025 katika ziara ya Mhe. Neale Richmond Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland ya kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa lengo la kuona maendeleo ya Mradi wa Maziwa Faida unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania unaotekelezwa na kituo cha TALIRI Tanga.

Akiongea kwa niaba ya wafugaji wengine Bw. Michael Simon amesema kupitia Mradi wa Maziwa Faida wamefanikiwa kupata mafunzo juu ya namna ya kutunza malisho kwa ajili ya kipindi cha kiangazi na utengenezaji wa robota za malisho kwa kutumia njia rahisi, mafunzo ya utunzaji wa ndama na elimu juu ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa kwa ujumla ili kupata tija kwenye ufugaji kutokana na ongezeko la maziwa.

“Tunajivunia sana na uwepo wa mradi huu tunaomba TALIRI iendelee kutekeleza mradi huu ili kufikia wafugaji wengi nchini kwani sasa tunafanya ufugaji wenye tija kutokana na mafanikio tunayopata kupitia mradi huu” Alisema Michael.

Kwa upande wake Prof. Erick Komba Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo amesema kupitia Mradi wa Maziwa Faida Taasisi imefanikiwa kuboresha miundombinu, kuendeleza ardhi kwa ajili ya kilimo cha malisho, uboreshaji wa mbari za mifugo kwa njia ya uhimilishaji, kutoa elimu ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa kwa wafugaji na kusomesha wataalamu wa Taasisi.

Prof. Komba emeendelea kutoa shukrani kwa Rais wa awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga mazingira rafiki ambayo yanawezesha wadau mbalimbali kuendelea kufadhili shughuli za utafiti wa mifugo.

Nae Prof. Riziki Shemdoe Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi amesema Wizara itaendelea kuhakikisha taasisi inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuweza kufikia malengo ya Mradi ya kuongeza mnyororo wa thamani wa ng’ombe wa maziwa kwa wafugaji nchini.

Akipongeza mara baada ya kupata maelezo juu ya shughuli zinazofanywa na mradi Mhe. Neale amesema amefurahishwa kwa namna TALIRI inatekeleza mradi huo na kuwa Ireland itaendelea kushirikiana na Taasisi hiyo na kuendelea kufadhili mradi huo.