Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
ZOEZI LA UTOAJI WA CHANJO NA UTAMBUZI WA MIFUGO LAANZA RASMI MKOANI MANYARA
21 Jul, 2025
ZOEZI LA UTOAJI WA CHANJO NA UTAMBUZI  WA MIFUGO LAANZA RASMI MKOANI MANYARA

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza rasmi kutekeleza Mpango kabambe wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Kitaifa, ambapo leo imetoa chanjo kwa mifugo takribani 400 ili kuboresha na kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Mifugo na kuondoa vikwazo ambavyo vimekuwa vikizuia mifugo na mazao yake kuuzwa katika nchi zenye masoko mazuri.

Akizungumza katika zoezi la Uhamasishaji na Utoaji Chanjo za Mifugo leo Julai 3, 2025 Wilayani Babati Mkoani Manyara, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Babati ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi wa zoezi la Uhamasishaji na Utoaji wa Chanjo za Mifugo Wilayani hapo, Ndg. Thobias Abwaro amesema zoezi la Utoaji Chanjo na Utambuzi wa Mifugo ni zoezi endelevu ambalo ni la muda mrefu na litaleta tija kwa wafugaji na Taifa zima kwa ujumla.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kugharamia Mpango wa Utoaji chanjo na Utambuzi wa Mifugo kwa miaka 5 kutoka 2025 hadi 2029, ambao utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 216 za Kitanzania, na ametoa ruzuku ya asilimia 100 kwa chanjo za kuku ambayo ni sawa na bure, na asilimia 50% kwa chanjo za ng’ombe na mbuzi/kondoo, ambapo ng’ombe ni tshs. 500/= na mbuzi/kondoo ni tshs. 300/=, hii yote ni kuonesha ni jinsi gani anajali Mifugo na Wafugaji.” ameseama Ndg. Abwaro

Aidha, Ndg. Abwaro amesema kwa muda mrefu uchanjaji wa Mifugo umekuwa ukifanyika kidogo kidogo katika ngazi za Mamlaka ya Serikali za Mitaa, mashamba makubwa na wafugaji mmoja mmoja bila kuwa na uratibu wa pamoja ambao hauwezi kutokomeza magonjwa ya mifugo, kwani ili kutokomeza maginjwa hayo inabidi kuchanja Mifugo angalau kwa asilimia 70%.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba, amesema kuwa Mifugo inaathiriwa sana na magonjwa ambayo yanapelekea vifo vya Mifugo na mazao yake kutokuwa bora na hata kupelekea kutokidhi viwango vya masoko ya nje.

“Ndio maana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia na kuiwezesha sekta hii ili kuboresha maisha ya wafugaji na kutanua wigo wa masoko ya nje” amesema Prof. Komba.

#taliriutafitikwamaendeleo