Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
WADAU WA MIFUGO WAKUTANA KUJADILI MIONGOZO YA KISERA
10 Oct, 2024
WADAU WA MIFUGO WAKUTANA KUJADILI MIONGOZO YA KISERA

Kupitia mradi wa ADGG ‘African Dairy Genetic Gains’ unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) tarehe 13/09/2024 walikutana na wadau mbalimbali wa mifugo wakiwemo viongozi toka wizara ya Mifugo na uvuvi, wataalamu elekezi toka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), wasindikaji maziwa na wafugaji kujadili miongozo ya kisera na kitaalamu itakayotumika kutambua na kuthibitisha ubora wa ng’ombe wa maziwa.

ADGG ni mradi wa kuboresha mbari za ng’ombe wa maziwa ambao unaohusika na kuandaa kanzidata, kutathmini na kuorodhesha aina ya ng’ombe bora wa maziwa kwa vigezo vya kitaalamu na kutoa elimu kwa wafugaji lengo ikiwa ni kumuwezesha mfugaji kunufaika na ufugaji wenye tija.

Katika kikao hicho kilichofanyika ndani ya ukumbi wa Rafiki Hoteli,Dodoma, kilihudhuliwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Angelo Mwilawa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kimejadili miongozo mbalimbali ili kupata vigezo vitakavyotumika kuthibitisha aina ya ng’ombe bora wa maziwa nchini.

Akiongea Dkt. Mwilawa amesema mradi wa ADGG umefanya kazi kubwa juu ya ufugaji wenye tija hivyo Wizara hiyo itaendelea kutoa ushirikano wakati wote na ameitaka TALIRI kuendelea kutekeleza mradi huo wenye tija kwa wafugaji kwa weledi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba amesema taasisi yake imejipanga kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa maslahi ya wafugaji na Taifa kwa ujumla na kwamba Taasisi itaandaa andiko la ushauri wa kisera (policy brief) likalo shauri juu ya uanzishwaji na utekelezaji wa viwango vya utambuzi na ithibati kwa ng’ombe bora wa maziwa nchini.