FAHAMU JINSI YA KUZALISHA MALISHO YA ALFALFA

Alfalfa (_Medicago Sativa_) ni moja ya malisho ya jamii ya mikunde ambayo yanatajwa kuwa ni malisho bora kwa mifugo ya kila aina kutokana na faida zake ikiwemo kuwa na virutubisho vingi vya aina mbalimbali kama vitamini A, B, C, D na K, Protein (18% CP), madini ya chuma na madini ya kopa, kuwa na mizizi inayoenda umbali wa mita 2 hadi 4 chini ya ardhi hivyo kuweza kustahimili ukame, kuwa na uwezo wa kustawi kwenye maeneo yenye viwango mbalimbali vya hali ya hewa na aina za udongo lakini pia yanaweza kudumu kwa muda zaidi ya miaka 12 shambani tangu kupandwa.
Katika kuandaa shamba hatua za maandalizi ya shamba hufanyika ikiwemo kuchagua eneo lenye udongo wenye rutuba na pH 6.2 - 7.5 au kuboresha udongo kwa kuweka mbolea ya samadi, kuchagua eneo lisilo na mmomonyoko wa udongo au lisilo tuamisha maji, kufyeka vichaka na miti kwani mimea hii hupunguza uzalishaji kwa kiasi kikubwa sana kwenye maeneo yenye kivuli, kutifua bila kuchimba udongo wa chini usio kuwa na rutuba na kutengeneza vitalu vya kusia mbegu.
Mbegu hupandwa kwenye vitalu au udongo uliosambazwa vizuri na wenye rutuba ya kutosha ambapo ekari moja hutumika kilo 5 hadi 6.5 kwa kuchora mistari kwenye tuta yenye kina cha milimita 10 hadi 15 na umbali wa sentimita 60 kati ya mstari na mstari kisha kusia mbegu iliyochanganywa na mchanga kwenye mistari na kufukia kwa udongo kidogo au kuacha bila kufikia pamoja na kumwagilia maji kuwezesha mbegu kushikana na udongo vizuri.
Mbegu ya Alfalfa huvunwa baada ya kuona 65% - 75% ya vikonyo zimekuwa na rangi ya ‘brown’ ambapo kitendo hiki hutokea ndani ya miezi minne hadi mitano baada ya kusia au kukata mbegu huvunwa kwa kuchambua zile zilizokomaa na kuzianika tayari kwa kutwanga, kupepetwa kisha kuhifadhiwa ambapo hekta moja huweza kuzalisha mbegu kati ya kilo 250 - 500 kutegemea aina ya utunzaji.
Uvunaji wa malisho hayo hufanyika baada ya siku 30 hadi 35 tangu kusia mbegu kisha baada ya mavuno ya kwanza yatavunwa tena kati ya wiki 5 - 7 na yanaweza kutoa kiasi cha tani 15 - 20 za malisho endapo yatatunzwa vizuri.
Ni muhimu kuzslisha mbegu hizo wakati wa kiangazi kwani uwepo wa mvua nyingi huathiri maua.