ELIMU YA MALISHO BORA YATOLEWA KWA VIONGOZI WA UBALOZI WA IRELAND NCHINI TANZANIA

Mkurugenzi wa Taaasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku (anaonekana akiongea) akiwaelezea Viongozi wa Ubalozi wa Ireland Nchini Tanzania masuala ya malisho ikiwa ni matokeo ya utafiti juu ya ugunduzi wa malisho bora kwa kanda ya mashariki.
Viongozi hao wakiongozwa na Naibu Mkuu wa Ushirikiano Hellen Counihan wakiwa kwenye Ofisi za TALIRI za kanda hiyo zilizopo Mkoani Tanga kwa lengo la kuona namna taasisi hiyo inatekeleza mradi wa maziwa faida unaofadhiliwa na ubalozi huo wamefanikiwa kujionea mambo makubwa yaliyofanywa na mradi huo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya taasisi, ununuzi wa vitendea kazi, uendelezaji wa elimu kwa wataalamu wa taasisi hiyo na utoaji wa elimu ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa kwa wafugaji kwa lengo la kuongeza mnyororo wa thamani wa maziwa.
Sambamba na hayo wameshuhudia wafugaji wakipatiwa elimu ya ufungaji wa robota za malisho huku wafugaji hao wakielezea kufurahishwa na uwepo wa mradi huo uliowezesha kuboresha hali zao za maisha.
Maziwa faida ni mradi unaotekelezwa kituo cha TALIRI Kanda ya Mashariki ndani ya Mkoa wa Tanga Wilaya ya Muheza pekee huku malengo yakiwa ni kuwezesha uwepo wa mradi huo maeneo yote nchini ili kuwezesha wafugaji wengi wa ng’ombe wa maziwa kufanya ufugaji bora na wenye kuwaletea manufaa.