Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
KONGAMANO LA UBUNIFU WA MANDHARI NA MIFUMO YA MAZINGIRA LAJADILI MUSTAKABALI WA KILIMO IKOLOJIA TANZANIA
08 Jun, 2026
KONGAMANO LA UBUNIFU WA MANDHARI NA MIFUMO YA MAZINGIRA LAJADILI MUSTAKABALI WA KILIMO IKOLOJIA TANZANIA

Mkurugenzi na Mratibu wa Mradi wa Kujenga Jamii Imara na Zenye Ustawi kupitia Mbinu Shirikishi za Kilimo Ikolojia katika Maeneo Kame ya Tanzania (RESCOMM), Dr. Anthony Whitbread akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo katika Kongamano la Ubunifu wa Mandhari na Mifumo ya Mazingira 2026 lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Rafiki, Dodoma. Kongamano hilo limewakutanisha maafisa wa serikali, watafiti, wakulima, wafugaji, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kwa lengo la kujadili matokeo ya mradi, kubadilishana uzoefu na kubaini mbinu bora za kusambaza teknolojia zilizothibitisha kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na mifugo. Washiriki wa kongamano hilo kwa pamoja walisisitiza umuhimu wa usimamizi endelevu wa mandhari za kilimo, uhifadhi wa rasilimali za asili, urejeshaji wa maeneo yaliyoharibika pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo na jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Inatarajiwa kuwa mapendekezo yatakayotokana na kongamano hilo yatachangia kuimarisha sera na mikakati ya maendeleo ya sekta za kilimo na mifugo, pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia endelevu kwa ajili ya kujenga jamii zenye ustahimilivu na maendeleo endelevu nchini.