Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MFAHAMU MBUZI BORA AINA YA MALYA BLENDED
19 Jul, 2024
MFAHAMU MBUZI BORA AINA YA MALYA BLENDED

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imefanya juhudi za kuwezesha kupatikana kwa mbuzi mwenye sifa ya kutoa maziwa na nyama kwa wingi katika mazingira ya mfugaji kwa kufanya tafiti na kuzalisha mbuzi bora aina ya Malya Blended.

Mbuzi huyo ni matokeo ya mchanganyiko wa mbuzi wa asili, Kamorai kutoka Pakistani na Boer kutoka Afrika ya Kusini huku lengo kubwa la kuzalisha mbuzi huyo likiwa ni kuwezesha wafugaji kupata mbuzi bora ili kuweza kuboresha lishe, kuongeza kipato na kuchangia malighafi za viwanda kutokana na matumizi ya ngozi na mazao mengine yanayotokana na mbuzi.

Sifa za mbuzi huyo ni uwezo wa kutoa nyama nyingi na maziwa mengi kati ya lita 1 hadi 2 kwa siku, huwa wanaweza kuzaa watoto mapacha, uwezo wa kukuwa haraka na kufikia uzito wa kilo 30 hadi 40 katika kipindi cha miaka miwili hadi mitatu, na uwezo wa kuzaa zaidi ya mara tatu katika kipindi cha miaka miwili.

Sambamba na hayo mbuzi huyo pia ana umbile kubwa kuliko mbuzi wa asili, ana uwezo wa kuhimili joto na magonjwa ya mifugo ukilinganisha na mbuzi kutoka nje ya nchi na wana uwezo wa kukua haraka ukilinganisha na mbuzi wengine.

Kama ilivyo kwa mbuzi wengine mbuzi hawa hulishwa mabaki ya mazao ya mashambani kama vile mahindi, uwele, mtama na maharage, lakini pia malisho yaliyopandwa, majani na matunda ya miti ya asili kama mpopote ‘Leucaena’ mkungugu na mtunduru.

Inashauriwa kuwa mfugaji anapaswa kuwa muangalifu katika kuhakikisha kuwa mbuzi hawazaliani katika ukoo kwani wakizaliana watoto wanaweza kuzaliwa wakiwa vilema, wanaweza kuwa dhaifu na kufa mapema lakini pia ukuaji wa wao utakuwa ni wa taratibu hivyo ili kuepusha tatizo hilo hakikisha kuwa dume halipandi watoto wake.

TALIRI imesambaza mbuzi hawa katika maeneo mbalimbali nchini, kikiwemo kituo cha TALIRI Mpwapwa, Kongwa, Mabuki na West Kilimanjaro.