Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
INTA WATEMBELEA TALIRI
26 Nov, 2024
INTA WATEMBELEA TALIRI

Wataalamu kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Teknolojia ya Kilimo ya Argentina alimaarufu kama INTA (Instituto Nacional de Tecnología Agropecuaria) tarehe 22/11/2024 wametembelea ofisi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa ajili ya kufuatilia majadiliano juu ya mradi unaotarajiwa kutekelezwa na TALIRI wa Kuboresha Teknolojia za Ufugaji katika maeneo kame na nusu kame nchini Tanzania.

Akiongea Fernando D kutoka INTA ameeleza kuwa madhumuni ya mradi huo ni kuimarisha uwezo wa kiufundi unaohitajika ili kuongeza uzalishaji katika mifumo ya ufugaji kwa wafugaji wadogo.

Fernando ameendelea kueleza kuwa mradi utawezesha kushughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo usambazaji mdogo wa malisho, kufuga kupita kiasi, utekelezaji wa mazoea yasiyofaa kwa usimamizi wa malisho na ukosefu wa mipango katika matumizi ya malisho.

“Mradi utabuni na kutekeleza mashamba ya majaribio kwa ajili ya usimamizi wa malisho huku ukizingatia idadi ya rasilimali katika ranchi na ufugaji mdogo” alisema Fernando.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba amesema hadi sasa tayari maeneo ya mashamba ya majaribio kwa ajili ya mbinu sahihi za usimamizi wa malisho yameshapatikana, mafunzo yametolewa kwa wadau mbalimbali juu ya usimamizi wa malisho kwa mifumo ya wafugaji wadogo na ranchi na warsha za kutambua mbinu zinazofaa juu ya uboreshaji wa malisho katika ufugaji kwa wafugaji wadogo na ranchi ili kuwezesha hatua za utekelezaji wa mradi.

Aidha, Mradi huo utatekelezwa nchini Tanzania na Kenya wakiwa ni wanufaika wakuu wa mradi, huku nchi ya Argentina ikiwa Mshirika Mkuu na Ujerumani ikiwa ni Mshiriki Mwezeshaji.