ILI UWEZE KUFUGA KWA TIJA UNAHITAJI KUWA NA MALISHO BORA, MANGESHO

“Bila malisho hakuna mifugo, wafugaji wengi wamekuwa wakifuga katika hali ya kawaida sisi tunataka tuwatoe huko na tuwaeleze kwamba ili uweze kufuga unahitaji kuwa na malisho ya kutosheleza mifugo yako kwa mwaka mzima”
Kauli hiyo imetolewa na Walter Mangesho Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam ndani ya banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi yakiwa na kauli mbiu isemayo, “Tanzania: Mahali Sahihi Pa Biashara Na Uwekezaji”
Mangesho ameendelea kueleza kuwa TALIRI imezalisha mbegu bora za malisho ya nyasi aina ya Cenchrus Ciliaris ambazo zimefanyiwa utafiti na kuonekana kufanya vizuri kwenye maeneo mengi nchini Tanzania kwani yana uwezo wa kustahimili ukame na hivyo kutoa matunda mazuri kwa wafugaji kwa maana ya kuongezeka kwa uzalishaji wa maziwa na nyama kutokana na viini lishe vilivyopo kwenye nyasi hizo.
Sambamba na hayo Mangesho ameeleza kuwa malisho haya yanauwezo wa kuzalisha na kutoa takribani tani 6 hadi 10 kwa ekari moja kwa mwaka na yanaweza kuoteshwa kwa kutumia njia ya vipando au kwa njia ya mbegu, pia yanaweza kuhifadhiwa katika hali ya ukavu yakiwa kwenye robota ‘hay’ na uzito wa takribani kilo 18 ambazo kwa wastani zinaweza kutumiwa na ng’ombe mmoja au wawili kwa siku huku ng’ombe wa maziwa mwenye uzito wa kilo 250 hadi 300 anaweza kula robota moja kwa siku mbili.
“Aina nyingine za nyasi zinaitwa Napier, mabingobingo na juncao ambazo zimeonekana kufanya vizuri kwenye maeneo yenye milima au sehemu zenye maji maji huku yakiwa na uwezo wa kuzalisha tani 8 hadi 16 kwa ekari moja kwa mwaka na ambazo zinaweza kutosheleza kulisha ng’ombe mmoja kwa mwaka.
Aidha, Mangesho ametoa wito kwa wadau wa mifugo kutembelea banda hilo ili kuweza kujifunza kwa undani elimu ya lishe na ulishaji wa mifugo pamoja na teknolojia mbalimbali za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mifugo yao.