KUKU WALIOBORESWA AINA YA HORASI WAVUTIA WANANCHI NANENANE

Kuku walioboreshwa aina ya HORASI wamekua kivutio kwa wananchi wanaotembelea mabanda ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma yanapoendelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo maarufu kama Nanenane.
Kuku hao wana uwezo wa kutaga mayai 200 hadi 240 kwa mwaka na kufikia uzito wa kg 1.5 ndani ya wiki 16.
Akiongelea kuku hao Bw. Onesmo Lyahama Mtaalamu kutoka TALIRI amesema kuwa Horas wana sifa ya kuwa na shingo na miguu mirefu, ukuaji wa haraka, uwezo wa kustahimili mazingira magumu na mwili mkubwa zaidi ukilinganisha na kuku wengine wa asili.
“Kuku hawa ni bora katika uzalishaji kwani kuku wengine wa asili wasioboreshwa hufikia uzito wa gramu 1,200 – 1,500 kwa mwaka na kutaga wastani wa mayai kati ya 30 - 45 kwa mwaka hivyo Horas wanaongeza tija ya ufugaji wa kuku wa asili nchini” Alisema Bw. Lyahama.
Naye Bw. Alex Msigwa Mfugaji wa kuku ambaye alipotembelea banda hilo na kupata elimu juu ya kuku hao amesema amefurahishwa na ubora wa kuku hao kuanzia muonekano wao kwani wanaonekana kuwa na miili mikubwa ukilinganisha na kuku wengine wa asili.
“Mimi nafuga kuku wa kienyeji ambao hawajaboreshwa na uzalishaji wake ni mdogo sana, hivyo nimenunua kuku hawa ambao ni jogoo na tetea ninategemea nitaenda kuboresha kuku wangu na kuwazalisha kwa wingi ili niweze kuongeza kipato changu, nimefurahi sana kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa TALIRI” Alisema Msigwa.
Kwa sasa kuku wa Horasi wanaendelea kufanyiwa majaribio katika kituo cha TALIRI Naliendele ambacho kinazalisha kuku hao kupitia teknolojia ya uhimilishaji ‘Artificial Insemination’ lengo ikiwa ni kuwa na uhakika wa taarifa za kitafiti kwa kila uzao.
Uzalishaji kwa wingi utaanza mara tu baada ya kukamilika kwa awamu za utafiti na kuku watasambazwa kwa wafugaji kote nchini ambapo kwa sasa kimeshapatikana kizazi cha awamu ya kwanza.