MKURUGENZI WA ILRI TANZANIA AVUTIWA NA TEKNOLOJIA ZA TALIRI
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) nchini Tanzania, Dkt. Anthony Whitbread, ametembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Samwel Malecela, jijini Dodoma, na kujionea teknolojia mbalimbali za kisasa zinazobuniwa na Taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya mifugo.
Akiwa katika banda hilo, Dkt. Whitbread amejionea teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na Taasisi hiyo, ikiwemo mbari za mifugo, malisho na mbegu za malisho, vyakula vya ziada vya mifugo, pamoja na teknolojia za uhimilishaji na uboreshaji wa mifugo zinazolenga kuongeza uzalishaji, tija na kipato cha wafugaji.
Dkt. Whitbread ameipongeza TALIRI kwa kazi kubwa ya kufanya tafiti zenye matokeo yanayoonekana na kwa juhudi zake za kuhakikisha teknolojia zinazozalishwa zinawafikia wafugaji kupitia maonesho, mafunzo na programu mbalimbali za uhamishaji wa teknolojia.
“Nimefurahishwa kuona ubunifu na teknolojia nyingi zinazozalishwa na TALIRI, Teknolojia hizi ni suluhisho muhimu kwa maendeleo ya sekta ya mifugo nchini. ILRI itaendelea kushirikiana na TALIRI katika tafiti, ubunifu na kujenga uwezo ili kuhakikisha teknolojia hizi zinawanufaisha wafugaji wengi zaidi,” alisema Dkt. Whitbread.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba amesema ushirikiano kati ya TALIRI na ILRI umeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha tafiti za mifugo nchini kupitia utekelezaji wa miradi ya pamoja, kubadilishana uzoefu wa kisayansi na kuendeleza teknolojia zinazowaletea manufaa wafugaji.
“TALIRI inaendelea kufanya tafiti zinazotoa majibu ya changamoto halisi za wafugaji. Ushirikiano wetu na ILRI umetuwezesha kuendeleza ubunifu, kujenga uwezo wa wataalamu na kuhakikisha teknolojia zinazozalishwa zinawafikia wafugaji kwa wakati ili kuongeza tija na kuchangia usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi,” alisema Prof. Komba.
