Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TUME YA HAKI ZA BINADAMU WATEMBELEA TALIRI
25 Jul, 2024
TUME YA HAKI ZA BINADAMU WATEMBELEA TALIRI

Watumishi kutoka Tume ya Haki za Binadamu wakiongozwa na Mhe. Kamishna Dkt. Thomas P Masanja wametembelea Ofisi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Makao Makuu kwa lengo la kupata maoni ya wataalamu wa taasisi hiyo yatakayowezesha kuandaliwa kwa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Biashara na Haki za Binadamu.

Akiongea Mhe. Kamishna Dkt. Masanja ameeleza kuwa maoni hayo yatatumika kuandaa mpango kazi huo ambao utawezesha kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa kwenye maeneo ya biashara mbalimbali zikiwemo za sekta ya mifugo.

Akitoa maoni Ndg. Joyce Sakaya ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo ameeleza kuwa TALIRI ina majukumu ya kubaini, kutathmini na kusambaza teknolojia mbalimbali za mifugo kwa lengo la kuongeza tija katika ufugaji huku ikiyatekeleza kwa kushirikiana na wafugaji na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Kwa upande wake Dkt. Daniel Komwihangilo Meneja wa Utafiti TALIRI ameeleza kuwa mbali na taasisi hiyo kutekeleza majukumu hayo lakini imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wafugaji juu ya utunzaji wa mazingira kwa kuwaeleza idadi sahihi ya mifugo ambayo mfugaji anapaswa kuwa nayo kutokana na ukubwa wa eneo lake kwani kuweka mifugo mingi kwenye eneo dogo kunapelekea uharibifu wa mazingira lakini pia kuwaelimisha wafugaji juu ya kuhakikisha mifugo yao inatoa kiasi kidogo cha hewa ya ‘methane’ na kubaki kuwa na uzalishaji mkubwa kwani hewa hiyo inapelekea kuharibu tabaka la juu la anga na hivyo kusababisha mabadiliko hasi ya tabia ya Nchi.

Dkt. Komwihangilo ameongeza kuwa taasisi hiyo inatekeleza shughuli zake kwa kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa kwa kutoa bidhaa bora za mifugo zilizotokana na teknolojia za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo ikiwemo malisho bora, mbari bora na vyakula vya mifugo ili kuongeza tija kwenye ufugaji pamoja na kufanya ‘Corporate Social Responsibility’ (CSR) yaani kurudisha kwa jamii kwa kuwapa wafugaji teknolojia hizo lakini pia kutoa elimu ya ufugaji bora.