Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MHE. ULEGA AITAKA TALIRI KUFANYA TAFITI ZA WANYAMA WADOGO
10 Oct, 2024
MHE. ULEGA AITAKA TALIRI KUFANYA TAFITI ZA WANYAMA WADOGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kufanya utafiti wa sungura akiwa ni moja kati ya wanyama wadogo wasiozoeleka kufugwa na wafugaji wengi.

Mhe. Ulega ametoa agizo hilo leo tarehe 07/08/2024 alipotembelea banda la taasisi hiyo ili kujionea namna ambavyo taasisi hiyo inatoa elimu kwa wafugaji na wadau wengine wa mifugo katika Maonesho ya 31 ya Kilimo ya Kimataifa (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika ndani ya viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’

Sambamba na hayo Mhe. Ulega ameipongeza TALIRI kwa namna ilivyojipanga katika kutoa elimu juu ya teknolojia bora za malisho na vyakula vya mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza tija ya ufugaji.

Akiongea Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Vitus Komba amesema katika maonesho hayo TALIRI imeendelea kutoa elimu juu ya mbari bora za mifugo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na mazao mengine ya mifugo pamoja na elimu ya mbegu bora za malisho na vyakula vya mifugo ikiwa ni teknolojia za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo.

Aidha, Prof. Komba ameeleza kuwa TALIRI ina mkakati wa kufanya utafiti kwa wanyama wasiozoeleka akiwemo sungura na punda ili kuhakikisha wanyama hao wanaendelea kutunzwa na kuwepo nchini na kwa sasa utafiti wa mnyama punda unaendelea kufanyika.

TALIRI inajukumu la kubaini, kutathmini na kusambaza teknolojia bora za mifugo na malisho nchini ili kuongeza tija kwenye ufugaji.