Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
SERIKALI YAIMARISHA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA
08 Jun, 2026
SERIKALI YAIMARISHA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Serikali imeendelea kuimarisha mikakati mbalimbali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia azma ya kuwa na Tanzania ya kijani, salama na yenye maendeleo endelevu. Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi wakati akihitubia katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Makamu wa Rais amesema kuwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za asili, kuhamasisha matumizi ya nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira, kuendeleza programu za upandaji miti, pamoja na kuimarisha mifumo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta mbalimbali za uchumi. Vilevile, amepongeza hatua zinazopatikana katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, akibainisha kuwa matumizi ya nishati safi yameongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2021 hadi asilimia 30 mwaka 2025, jambo linalochangia kupunguza utegemezi wa nishati zinazoharibu mazingira. Katika maadhimisho hayo, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ilishiriki maonesho ya maadhimisho kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu teknolojia na mbinu mbalimbali za uhifadhi wa mazingira zinazochangia maendeleo ya sekta ya mifugo na kukuza ufugaji wenye tija, endelevu na unaohimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Wananchi waliotembelea banda la TALIRI walipata fursa ya kujifunza kuhusu matumizi ya nishati safi kupitia teknolojia ya biogesi inayozalishwa kutokana na kinyesi cha mifugo, pamoja na namna teknolojia hiyo inavyosaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuboresha afya za jamii na kuhifadhi mazingira. Aidha, walielimishwa kuhusu matumizi ya mbolea za asili zinazotokana na mifugo na mchango wake katika kuimarisha uzalishaji wa mazao na afya ya udongo.