Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MITI MALISHO CHAKULA CHA ZIADA KWA MIFUGO
10 Oct, 2024
MITI MALISHO CHAKULA CHA ZIADA KWA MIFUGO

Wanyama wanahitaji chakula kinachowapa nguvu, protini na madini kwa ajili ya kujenga na kulinda miili yao hivyo kuwawezesha kukua vizuri na kutoa nyama nyingi na maziwa mengi zaidi.

Majani wanayokula mifugo huwapa nguvu lakini yana kiwango kidogo cha protini na madini, pia viini lishe hupungua sana wakati wa kiangazi kwa sababu majani huwa yamekomaa na kukauka, katika hali hiyo inabidi kumpa mnyama vyakula vya ziada ili aweze kukua vizuri na kuandaliwa kuwa mzazi mwenye uzazi na uzalishaji mzuri wa maziwa, hivyo njia rahisi ni kupanda miti malisho jamii ya mikunde kama vile Milusina, Glirisidia, Moringa, Sesbania na Mbaazi ambayo ina viinilishe vingi na bora kwa ajili ya mifugo.

Mbali ya kuwa na viini lishe kupanda miti malisho kuna faida nyingi ikiwemo kuokoa muda wa kwenda kutafuta malisho, kuongeza ubora wa chakula na kupunguza matumizi ya chakula cha ziada kama pumba na mashudu, kuzuia mmomonyoko wa udongo, kuongeza pato kwa kuuza mbegu na miche ya miti malisho na kuwezesha wanyama kukua haraka hivyo kuweza kutoa maziwa na nyama nyingi na kupelekea kufikia bei ya soko.

Lakini pia miti malisho ina sifa mbalimbali ikiwemo kukua haraka na kutoa malisho mengi, ina protini nyingi zaidi ya nyasi hivyo hutumika kama chakula cha ziada, huweza kukatwa mara kwa mara hivyo kutoa malisho nyakati tofauti, inaweza kuoteshwa pamoja na mazao mengine.

Lakini pia inaweza kusindikwa na kutumiwa wakati wa uhaba wa malisho kama wakati wa kiangazi, huvumilia ukame, faida za ziada ni pamoja na kuboresha ardhi na maua ya miti malisho kama Calliandra ni kivutio kizuri cha nyuki.

Miti malisho inaweza kupandwa kwenye mipaka ya shamba au ndani ya shamba, eneo la kuzunguka nyumba kama uzio, maeneo maalum kama vishamba vidogo vidogo, katika miinuko shambani na kwenye matuta ya kuzuia mmomonyoko wa udongo.