Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
WAZIRI WA FEDHA AIPONGEZA TALIRI KWA USAJILI WA MBEGU ZA MALISHO, ASEMA ZITASAIDIA KUPUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI
10 Aug, 2026
WAZIRI WA FEDHA AIPONGEZA TALIRI KWA USAJILI WA MBEGU ZA MALISHO, ASEMA ZITASAIDIA KUPUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Musa Omar (Mb), ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa mafanikio ya kusajili mbegu za malisho, hatua aliyoeleza kuwa ni muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa mifugo na kupunguza migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Mhe. Balozi Omar ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya John Samwel Malecela, jijini Dodoma. Akiwa banda hilo, alipata fursa ya kujionea huduma na teknolojia mbalimbali zinazozalishwa na taasisi hiyo, zikiwemo mbari bora za mifugo, malisho na mbegu za malisho, pamoja na teknolojia za utengenezaji wa vyakula vya ziada vya mifugo.

Aidha, Waziri huyo ameipongeza TALIRI kwa kuendelea kufanya utafiti na kubuni teknolojia zinazolenga kuongeza tija, uzalishaji na kipato cha wafugaji nchini.

“Nimeona mafanikio makubwa katika eneo la malisho. Kwa mfano, malisho ya Juncao yana uwezo wa kuzalisha hadi tani 60 kwa ekari moja. Hii ni hatua kubwa itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa malisho na kupunguza migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi,” amesema Mhe. Balozi Omar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick V. Komba, amesema Taasisi inaendelea kutekeleza mpango wa kuwawezesha wadau mbalimbali kuzalisha mbegu za malisho, huku TALIRI ikibaki kuwa mzalishaji wa mbegu mama ili kuhakikisha ubora wa mbegu unaendelea kuzingatiwa.

Prof. Komba amesema kuwa TALIRI pia imeongeza uwekezaji katika uzalishaji wa teknolojia mbalimbali za mifugo, ikiwemo kupanua maeneo ya uzalishaji wa malisho, kuongeza uzalishaji wa mbegu za malisho na kuzalisha idadi kubwa zaidi ya mifugo bora kwa ajili ya kusambazwa kwa wafugaji nchini.

Ameongeza kuwa juhudi hizo zina lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo, kuboresha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wafugaji na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya mifugo.