Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
DKT. MADELE AITAKA TALIRI KUONGEZA UZALISHAJI WA MALISHO KUKABILIANA NA KIANGAZ
21 May, 2026
DKT. MADELE AITAKA TALIRI KUONGEZA UZALISHAJI WA MALISHO KUKABILIANA NA KIANGAZ

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele, ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuongeza juhudi za uzalishaji na uhifadhi wa malisho ya mifugo ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa malisho kipindi cha kiangazi.

Dkt. Madele ametoa maelekezo hayo leo Mei 19, 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo cha TALIRI Kanda ya Mashariki kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali za utafiti na maendeleo zinazotekelezwa na taasisi hiyo.

Amesema upatikanaji wa malisho bora na ya kutosha ni msingi muhimu wa kuongeza tija katika sekta ya mifugo, hivyo ni muhimu TALIRI kuendelea kufanya tafiti na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa za uzalishaji wa malisho ili kuwasaidia wafugaji kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa kunakuwa na mkakati wa kudumu wa uzalishaji na uhifadhi wa malisho ili wafugaji wasiendelee kuathirika kila kipindi cha ukame. Tafiti zinazofanywa hapa zinapaswa kuleta suluhisho la moja kwa moja kwa wafugaji wetu,” amesema Dkt. Madele.

Aidha, ameitaka taasisi hiyo kuhakikisha inaweka mikakati thabiti ya matumizi bora ya ardhi inayomilikiwa na kituo hicho ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za kitafiti pamoja na kuimarisha uzalishaji wenye tija kwa maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika tafiti za malisho bora, uhifadhi wa chakula cha mifugo pamoja na teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza uzalishaji wa mifugo nchini.

Prof. Komba amesema TALIRI itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha matokeo ya tafiti yanafika kwa wafugaji kwa wakati na kusaidia kuongeza uzalishaji, kipato cha wafugaji na usalama wa chakula.

“TALIRI tunaendelea kubuni na kusambaza teknolojia mbalimbali za ufugaji zenye tija, ikiwemo uzalishaji wa malisho bora na mbegu zake, ili kuhakikisha wafugaji wanakuwa na mifugo yenye afya na uzalishaji wenye tija katika mazingira yote ya hali ya hewa,” amesema Prof. Komba.