Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MKUU WA MKOA WA DODOMA ATEMBELEA BANDA LA TALIRI DODOMA
06 Aug, 2024
MKUU WA MKOA WA DODOMA ATEMBELEA BANDA LA TALIRI DODOMA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Sitaki Senyamule ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuendelea kusambaza elimu ya malisho bora kwa wafugaji wa Mkoa huo ili kuwawezesha kufanya ufugaji wenye tija kwa kuwa na uhakika wa chakula kwa mifugo yao sambamba na kupunguza migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Mhe. Senyamule ametoa kauli hiyo leo tarehe 04/08/2024 alipotembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya 31 ya Kilimo ya Kimataifa ‘Nanenane’ ambayo kitaifa yanafanyika Kanda ya Kati ndani ya viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’

Sambamba na hayo Mhe. Senyamule ameipongeza taasisi hiyo kwa jinsi ilivyojipanga kutoa elimu ya teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na taasisi hiyo kwa wafugaji na wadau mbalimbali wa mifugo.

Akiongea Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick V Komba ameeleza kuwa TALIRI ni taasisi inayofanya tafiti mbalimbali za mifugo ikiwa na jukumu la kuibua, kutathmini na kusambaza teknolojia bora za malisho na uzalishaji wa mifugo.

Prof. Komba ameendelea kueleza kuwa TALIRI imejipanga kusambaza teknolijia zake ikiwemo ya mbari bora za mifugo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na mazao mengine ya mifugo na mbegu bora za malisho na vyakula vya mifugo kwa wafugaji na wadau wote wa mifugo nchini.

Aidha, Prof. Komba ameeleza kuwa taasisi hiyo mbali na kutoa elimu hizo lakini pia wadau watafanikiwa kujionea namna teknolojia hizo zinafanya kazi kwa vitendo ikiwemo teknolojia ya uhimilishaji wa kuku.

Tambua kuwa TALIRI inashiriki Maonesho haya kwenye kanda zote nchini ili kutoa fursa kwa wafugaji kupata elimu hizo.