Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TEKNOLOJIA NA TAKWIMU ZA KIDIJITALI MUHIMU KATIKA UBORESHAJI WA VINASABA VYA NG’OMBE WA MAZIWA
25 Jun, 2026
TEKNOLOJIA NA TAKWIMU ZA KIDIJITALI MUHIMU KATIKA UBORESHAJI WA VINASABA VYA NG’OMBE WA MAZIWA

 

Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Vinasaba vya Ng’ombe wa Maziwa katika Ukanda wa Kitropiki (TDGG), Dkt. Eliamoni Lyatuu kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), amesema matumizi ya teknolojia za kisasa na takwimu za kidijitali ni muhimu katika kuharakisha uboreshaji wa vinasaba vya ng’ombe wa maziwa na kuongeza tija kwa wafugaji wadogo nchini.

Dkt. Lyatuu alitoa kauli hiyo Juni 23, 2026, wakati wa warsha iliyofanyika katika ukumbi wa Panama Hoteli mkoani Kilimanjaro iliyowakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo watunga sera, taasisi za serikali, watafiti, washirika wa maendeleo, wafugaji wadogo na wa kibiashara, vyama vya ushirika, wasindikaji wa maziwa, maafisa ugani pamoja na wasambazaji wa pembejeo za mifugo.

Warsha hiyo ililenga kujadili uwezo na matumizi ya mfumo wa Mradi wa TDGG, kujenga uelewa wa pamoja kuhusu shughuli zinazotekelezwa na mradi huo, pamoja na kuweka mikakati ya kuendeleza na kupanua matumizi ya mfumo huo ili kuwafikia wafugaji na wadau wengi zaidi nchini.

Akizungumza katika warsha hiyo, Dkt. Lyatuu alisema kuwa mradi huo, unaofadhiliwa na Wakfu wa Bill na Melinda Gates na kutekelezwa na ILRI kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), unalenga kuzijengea nchi za kitropiki mifumo madhubuti ya kitaifa ya ukusanyaji na usimamizi wa takwimu za mifugo.

Alisema mradi huo pia unahamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kufuatilia uzalishaji wa mifugo na kuwezesha uandaaji wa viwango vya kitaifa vya uchaguzi wa mifugo bora kwa ajili ya kuzalisha kizazi chenye tija kubwa zaidi.

“Ili kufanikisha hilo, mradi umeanzisha na kuendeleza mfumo wa TDGG wa usimamizi wa takwimu za mifugo unaowezesha ukusanyaji, uhifadhi, uchambuzi na matumizi ya taarifa za mifugo kwa njia ya kidijitali,” alieleza Dkt. Lyatuu.

Kwa upande wake, Afisa TEHAMA wa mradi huo kutoka ILRI, Bi. Neema Kelya, alisema mfumo huo umewezesha usajili na ufuatiliaji wa mifugo kuanzia kuzaliwa hadi kuondolewa kwenye uzalishaji, huku ukiruhusu kurekodi matukio mbalimbali yakiwemo makuzi ya ndama, uzazi, uhimilishaji, afya, lishe na uzalishaji wa maziwa.

Bi. Kelya aliongeza kuwa mfumo huo, ambao unatarajiwa kuunganishwa na mfumo wa utambuzi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, unawahudumia wadau mbalimbali wakiwemo wafugaji, vyama vya ushirika, taasisi za utafiti, vyuo vya elimu ya juu, watoa huduma za uhimilishaji, wazalishaji na wasambazaji wa mbegu bora za mifugo, maafisa ugani, watunga sera, taasisi za kifedha, wasambazaji wa pembejeo za mifugo, wasindikaji wa maziwa, wawekezaji, wakusanyaji na wasafirishaji wa maziwa.

Alisema kuwa kwa upande wa wafugaji, mfumo huo utawawezesha kufanya maamuzi sahihi kwa kupata taarifa za wakati halisi kuhusu mifugo yao, ikiwemo kiwango cha uzalishaji wa maziwa, hali ya lishe, uzazi pamoja na ushauri wa kitaalamu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Sehemu ya Usimamizi, Uzalishaji na Uendelezaji wa Mbari za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Jeremia Temu, pamoja na Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Prof. George Msalya, walipongeza hatua iliyofikiwa na Mradi wa TDGG kwa kuanzisha mfumo huo wa kidijitali.

Viongozi hao walisema mfumo huo ni chachu ya kuimarisha sekta ya maziwa nchini kwa kuwa unasaidia upatikanaji wa takwimu sahihi na za kuaminika, zinazowezesha kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kuchagua mifugo bora na kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa pamoja na kuimarisha ushindani wa sekta hiyo ndani na nje ya nchi.

Aidha, walisisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika matumizi na uendelezaji wa mfumo huo ili kuhakikisha manufaa yake yanawafikia wafugaji wengi zaidi na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya mifugo nchini