SERIKALI YAITAKA TALIRI KUIMARISHA TAFITI ZENYE TIJA KUKUZA SEKTA YA MIFUGO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo), Dkt. Fabian Madele, ameielekeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuendelea kufanya tafiti zenye tija zitakazotoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo nchini.
Dkt. Madele ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akifungua kikao cha saba cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TALIRI kilichofanyika katika ukumbi wa Vizano Hotel, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
Amesema kuwa mwelekeo wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuifanya sekta ya mifugo kuwa ya kibiashara, yenye ushindani ndani na nje ya nchi, na yenye manufaa kwa wafugaji pamoja na taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa ili kufikia azma hiyo, TALIRI ina jukumu la kuhakikisha wafugaji wanapata teknolojia bora za mifugo ikiwemo malisho bora na mbari zenye tija za mifugo.
Aidha, Dkt. Madele amesema Wizara itaendelea kuhakikisha tafiti za mifugo na malisho zinafanyika kwa kuzingatia weledi, ubunifu na ufanisi, ili kuleta matokeo chanya kwa wadau wa sekta hiyo. Pia ameielekeza taasisi hiyo kupanga bajeti yenye tija itakayowezesha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 hadi Machi 31, 2026, taasisi imefanikiwa kuwafikia wafugaji 6,051 katika maeneo mbalimbali nchini kwa kusambaza teknolojia bora za malisho na mbari za mifugo.
Ameongeza kuwa TALIRI imeendelea kuhifadhi na kuendeleza mbari za asili za mifugo zenye sifa muhimu kama ukuaji mzuri, uwezo wa kuhimili magonjwa, na uzalishaji kwa ajili ya tafiti na matumizi ya baadaye.
Prof. Komba pia amesema taasisi itaendelea kuandaa maandiko ya miradi ya utafiti ili kuwezesha upatikanaji wa fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.
Nae Meneja wa Sehemu ya Mipango, Bw. Benard Francis, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, TALIRI inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi Bilioni 13.1 (Tsh 13,109,646,600.00), sawa na ongezeko la asilimia 3.5 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/2026.
Amefafanua kuwa mchanganuo wa bajeti hiyo unajumuisha mapato ya ndani ya taasisi, ruzuku ya matumizi mengineyo, mishahara, pamoja na fedha za miradi ya maendeleo.
Aidha, amesema utekelezaji wa bajeti hiyo utazingatia maeneo ya vipaumbele ya utafiti yakiwemo malisho na mbegu zake, mbari za mifugo, lishe ya mifugo, afya ya mifugo, matumizi ya virutubisho asilia, pamoja na ustawi na haki za mifugo, sambamba na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta hiyo.
