NAIBU KATIBU MKUU WIZARANYA FEDHA APONGEZA TEKNOLOJIA YA JIWE LISHE TALIRI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anayeshughulikia Huduma za Hazina, Bw. Nsubili Joshua, ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa kuendelea kubuni na kuendeleza teknolojia mbalimbali za kisasa zinazochochea maendeleo ya sekta ya mifugo, hususani teknolojia ya Jiwe Lishe, ambayo amesema ina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji na kuboresha afya ya mifugo nchini.
Bw. Joshua ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, jijini Dodoma, ambapo alipata fursa ya kujionea teknolojia mbalimbali zinazozalishwa na Taasisi hiyo pamoja na kupata maelezo kuhusu matumizi na manufaa yake kwa wafugaji.
Amesema teknolojia zinazozalishwa na TALIRI zina nafasi muhimu katika kuimarisha tija ya sekta ya mifugo kwa kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na bidhaa nyingine za mifugo, huku zikiwasaidia wafugaji kuongeza kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Ubunifu huu wa Jiwe Lishe ni mfano mzuri wa namna ambavyo utafiti unaweza kutoa suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto zinazowakabili wafugaji. Ni muhimu teknolojia hizi ziendelee kuwafikia wafugaji wengi zaidi ili waweze kunufaika na matokeo ya tafiti zinazofanywa na TALIRI,” amesema Bw. Joshua.
Aidha, Bw. Joshua amewataka wataalamu wa TALIRI kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia zinazozalishwa na Taasisi, akisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia za kisasa ni nguzo muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Akitoa ufafanuzi kuhusu teknolojia ya Jiwe Lishe, mtaalamu wa TALIRI, Bw. Jovith Kajuna, amesema jiwe hilo limezalishwa kwa lengo la kumwezesha mfugaji kutumia jiwe moja lenye mchanganyiko wa viini lishe muhimu, ikiwemo madini, protini na wanga, vinavyohitajika na mifugo kwa wakati mmoja.
Bw. Kajuna amesema matumizi ya Jiwe Lishe husaidia kufidia upungufu wa madini mwilini, kuongeza hamu ya kula, kuboresha mmeng’enyo wa chakula, kuimarisha afya ya mifugo, kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama.
