Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
NAIBU KATIBU MKUU AITAKA TALIRI KUONGEZA UZALISHAJI WA JIWE LISHE KWA KIWANGO CHA KIBIASHARA
13 Jul, 2026
NAIBU KATIBU MKUU AITAKA TALIRI KUONGEZA UZALISHAJI WA JIWE LISHE KWA KIWANGO CHA KIBIASHARA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Prof. Mohamed Ali Sheikh, ameielekeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuongeza uzalishaji wa teknolojia ya jiwe lishe kwa kiwango cha kibiashara ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya wafugaji nchini, kufuatia mwitikio mkubwa wa bidhaa hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba). Prof. Sheikh ametoa maelekezo hayo leo Julai 12, 2026, alipotembelea banda la TALIRI katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo pia ameipongeza taasisi hiyo kwa jitihada za kuendelea kusambaza jiwe hilo kwa wafugaji. Akiwa katika banda hilo, Prof. Sheikh alipata fursa ya kujionea teknolojia mbalimbali zinazotolewa na TALIRI kwa wananchi na kueleza kuridhishwa na mwitikio mkubwa wa wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo, hususani katika matumizi na uhitaji wa jiwe lishe. Amesema kiwango kikubwa cha uuzaji wa jiwe lishe ni kiashiria cha mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo, hivyo kuna umuhimu wa TALIRI kuimarisha uzalishaji wake kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa wafugaji wengi zaidi nchini. “Nilipofika katika banda hili nilikuta mawe lishe mengi, lakini sasa yote yamekwisha kuuzwa. Hii inaonesha wazi kuwa mahitaji ya bidhaa hii ni makubwa. TALIRI iangalie uwezekano wa kuongeza uzalishaji wa jiwe lishe kwa kiwango cha kibiashara ili kukidhi mahitaji ya wafugaji,” amesema Prof. Sheikh. Kwa upande wake, Mtafiti kutoka TALIRI, Bw. John Diyu, amesema taasisi hiyo imepokea maelekezo hayo na itaendelea kuboresha uzalishaji wa mawe lishe kwa kuongeza uwezo wa uzalishaji pamoja na kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wakati ili kuwahudumia wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo. Aidha, Bw. Diyu amesema TALIRI itaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya teknolojia ya jiwe lishe, ambayo huchangia kuboresha lishe ya mifugo kwa kuongeza upatikanaji wa madini na virutubisho muhimu vinavyoongeza afya ya mifugo, uzalishaji wa maziwa na nyama, pamoja na tija kwa ujumla.