NG'OMBE ANAEFANYA VIZURI KWENYE KANDA KAME

Katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere, jijini Dar es salaam yakienda sambamba na kauli mbiu isemayo ‘Tanzania: Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji’ watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) leo tarehe 04/07/2024 wameendelea kutoa elimu juu teknolojia za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo kwa wadau wa mifugo wanaotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Akielezea ng’ombe aina ya Mpwapwa ikiwa ni moja ya teknolojia zilizoibuliwa na taasisi hiyo Bw. Gilbert Msuta Meneja wa Sehemu ya Teknolojia na Uhaulishaji amesema ng’ombe huyo ni matokeo ya utafiti uliolenga kumuwezesha ng’ombe kuzalisha nyama na maziwa kwa wingi katika mazingira kame.
Ng’ombe huyo aliyepatikana kwa mchanganyiko wa ng’ombe aina ya Ayrshire kutoka bara la Ulaya, Red - sindh na Sahiwal kutoka Asia , Boran na ng’ombe wa asili ana uwezo wa kustahimili mazingira ya ukame, kutoa maziwa kati ya lita 6 hadi 9 katika mazingira ya ukame ambayo ni zaidi ya mara nne ya maziwa anayotoa ng’ombe wa asili huku madume yakiwa na uwezo wa kutoa nyama kiasi cha kilo 250 wakiwa na umri wa miaka minne kiasi ambacho ni mara mbili ukilinganisha na ng’ombe wa asili.
Aidha, Msuta ametoa wito kwa wafugaji wanaofuga kwenye mazingira yenye ukame kutumia madume ya ng’ombe aina ya Mpwapwa au kutumia mbegu zake kwa njia ya uhimilishaji ili kupata ng’ombe chotara kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji wa nyama na maziwa kwenye ng’ombe wa asili.
Msuta ameongeza kuwa matunzo ya ng’ombe huyo ni ya gharama nafuu ukilinganisha na ng’ombe wa kigeni kwani anaweza kuchungwa na ana uwezo wa kustahimili magonjwa.
Wadau wameonesha kufurahishwa na elimu hiyo ambayo itaenda kuongeza tija ya ufugaji katika mazingira yenye ukame.