MWENDELEZO WA ZIARA YA UBALOZI WA IRELAND NCHINI TANZANIA

Ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Viongozi wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania leo tarehe 24/10/2024 Viongozi hao wamewatembelea wafugaji wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga wanaonufaika na Mradi wa Maziwa Faida unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki na kujionea mambo mazuri yanayofanywa na wafugaji hao kutokana na elimu ya ufugaji bora wanayopatiwa na wataalamu wa taasisi hiyo.
Pamoja na kutembelea wafugaji hao viongozi hao wamefanikiwa kujionea shamba darasa linalotumiwa na wafugaji hao kwa ajili ya kupata elimu kwa vitendo juu ya upandaji wa malisho na kutembelea kituo cha kukusanya maziwa kwa kuuzwa.
Akiongea Naibu Mkuu wa Ushirikiano wa ubalozi huo Suzanne Keatinge amesema mara nyingi suala la mafunzo huwa ni jambo gumu kwani na kuna muda wafundishwaji husinzia wakati wa kufundishwa lakini kwa wafugaji hao ameiona imekuwa tofauti kwani wameonekana kuwa na ari kubwa ya kufurahia na kuyaelewa mafunzo kutokana na matokeo chanya aliyoyaona juu ya ufugaji wao na ameipongeza timu ya TALIRI kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa wafugaji hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Komba amesema TALIRI itaendelea kuhakikisha elimu ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa inaendelea kuwafikia wafugaji na milango ipo wazi muda wote kwa wafugaji na wadau wengine wa mifugo kutembelea taasisi hiyo pale wanapohitaji kupata majibu juu ya masuala ya mbalimbali ya mifugo na ameushukuru ubalozi huo kwa kuwezesha mradi muhimu kwa wafugaji na Taifa kwa ujumla.
Nae mmoja kati ya wafugaji hao Ndg. Lightness ameishukuru TALIRI kwa kuwapatia mafunzo juu ya ufugaji wenye tija ikiwemo elimu ya malisho bora, kujua joto la ng’ombe, ufungaji wa robota za malisho ambapo sasa amejua robota moja ambalo huwa na uzito wa kilo ishirini wanaweza kula ng’ombe wawili wenye uzito wa kilo 300 kwa siku pamoja na elimu ya utunzaji bora wa ndama.
“Wakati natumia malisho ya asili nilikuwa napata maziwa lita 15 kwa siku kwa ng’ombe mmoja lakini tangu nimejifunza na kuzingatia juu ya malisho bora ya mifugo sasa napata lita 25 kwa siku kwa ng’ombe mmoja kitendo ambacho kimeniwezesha kuboresha maisha yangu na familia yangu” alisema Lightness.