WANANCHI WANUFAIKA NA TEKNOLOJIA ZA MALISHO BORA KUPITIA MASHAMBA DARASA YA TALIRI
Wananchi na wafugaji waliotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma, wameendelea kunufaika na elimu ya vitendo kuhusu uzalishaji na matumizi ya malisho bora ya mifugo kupitia mashamba darasa yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI).
Mashamba darasa hayo yamekuwa miongoni mwa maeneo yanayotoa fursa kwa wafugaji, wadau na wananchi kujifunza kwa vitendo teknolojia mbalimbali za uzalishaji wa malisho bora, ikiwemo namna ya kuzalisha, kutunza na kutumia malisho kwa kuzingatia mahitaji ya mifugo.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, Mtaalamu wa TALIRI, Bw. Emanuel Kisinga, amesema uwepo wa mashamba darasa unalenga kuwajengea uwezo wafugaji na wananchi kwa kuwaonesha kwa vitendo teknolojia zinazoweza kutumika katika uzalishaji wa malisho yenye ubora na virutubisho vya kutosha.
Amesema upatikanaji wa malisho bora na ya kutosha ni msingi muhimu katika kuongeza uzalishaji na tija ya mifugo, kwani huchangia kuboresha afya na ukuaji wa mifugo, kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama, pamoja na kupunguza changamoto ya uhaba wa chakula cha mifugo, hususani katika vipindi vya ukame.
Kisinga amesema elimu inayotolewa kupitia mashamba darasa hayo haitaishia kwenye kipindi cha Maonesho ya Nanenane pekee, bali TALIRI itaendelea kutoa mafunzo, ushauri na huduma za kitaalamu kwa wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo kwa mwaka mzima.
Ameeleza kuwa huduma hizo zitaendelea kutolewa kupitia mashamba darasa hayo na vituo vya utafiti vya TALIRI vilivyopo katika kanda mbalimbali nchini, hatua inayolenga kusogeza teknolojia za utafiti karibu na wananchi na kuwawezesha kuzitumia kulingana na mazingira na mahitaji ya maeneo yao.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliotembelea mashamba darasa hayo wamepongeza TALIRI kwa kutumia njia ya vitendo katika kutoa elimu, wakieleza kuwa imewawezesha kuelewa kwa urahisi namna ya kuzalisha na kutumia malisho bora katika shughuli zao za ufugaji.
