Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
CAG AITAKA TALIRI KUONGEZA UZALISHAJI WA JIWE LISHE KWA MASHINE ZA NDANI
10 Aug, 2026
CAG AITAKA TALIRI KUONGEZA UZALISHAJI WA JIWE LISHE KWA MASHINE ZA NDANI

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ndg. Charles Kichere, ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa ubunifu wa teknolojia ya Jiwe Lishe na kuitaka Taasisi hiyo kutumia mashine zinazotengenezwa nchini ili kuongeza uzalishaji wa teknolojia hiyo na kuwafikia wafugaji wengi zaidi.

Ndg. Kichere ametoa rai hiyo wakati Agosti 07, 2026 alipotembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma, ambapo alijionea teknolojia mbalimbali za mifugo zilizozalishwa na Taasisi hiyo kupitia tafiti zake.

Amesema TALIRI inapaswa kutumia fursa ya uwepo wa wazalishaji wa mashine nchini, ikiwemo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), ili kupata mashine zinazoweza kutumika katika uzalishaji wa Jiwe Lishe kwa wingi.

Aidha, CAG ameitaka TALIRI kuongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa Jiwe Lishe ili kuwafikia wafugaji wengi zaidi, akieleza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kuchangia kuongeza tija ya mifugo na kipato cha wafugaji.

Akielezea teknolojia hiyo, Mtaalamu kutoka TALIRI, Bw. Jovith Kajuna, amesema Jiwe Lishe ni miongoni mwa teknolojia zilizobuniwa na Taasisi hiyo kwa lengo la kukidhi mahitaji ya virutubisho muhimu kwa mifugo.

“Jiwe Lishe lina virutubisho muhimu kwa mifugo, ikiwemo madini, protini na nishati, tofauti na mawe mengine ambayo hutoa madini pekee. Matumizi yake husaidia kuongeza tija ya mifugo na hatimaye kuongeza kipato cha mfugaji,” amesema Bw. Kajuna.

Bw. Kajuna amesema teknolojia hiyo inalenga kuwawezesha wafugaji kupata virutubisho muhimu kwa mifugo yao kwa njia rahisi, huku ikisaidia kuboresha uzalishaji na ufanisi wa ufugaji.

TALIRI itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani, ikiwemo SIDO, katika kuendeleza na kuzalisha teknolojia zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji nchini.