WAFUGAJI WAASWA KUACHA KUTIBU MIFUGO KIHOLELA

Mtaalamu wa afya ya wanyama Ndg. Jackson Nkyami wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kituo cha Mpwapwa amewataka wafugaji kuacha tabia ya kutibu mifugo yao wenyewe na kutafuta msaada kutoka kwa wataalamu wa tiba ya mifugo kwani kitendo cha kuchukua maamuzi ya kutibu bila kuwa na utaalamu kinaweza kusababisha usugu wa vimelea dhidi ya dawa, vifo kwa mifugo kutokana na kuzidisha dozi na madhara mengine kama kudhoofu kwa mifugo na kupelekea kupoteza ubora wa soko la mifugo hiyo.
Hayo ameyasema akiwa na wataalamu wa taasisi hiyo walipotembelea wafugaji wa Wilaya ya Mpwapwa wa Kata ya Pwaga kijiji cha Pwaga kwa lengo la kuwapatia elimu juu ya ufugaji wenye tija ikiwa ni muendelezo wa programu za uhamasishaji ‘outreach program’ zinazofanywa na taasisi hiyo.
Sambamba na hilo Nkyami amewataka wafugaji hao kuzingatia utoaji wa chanjo muhimu kwa mbuzi na ng’ombe zikiwemo; homa ya mapafu ya ng’ombe (CBPP), homa ya mapafu ya mbuzi (CCPP), mapele ngozi (LUMPY SKIN), ugonjwa wa midomo na miguu (FMD), kimeta na chambavu (BRATHRAX) na sotoka ya mbuzi (PPR) kwa ajili ya kulinda mifugo kutopata magonjwa yatakayopelekea kupunguza mitaji ya wafugaji.
Akiongezea kwenye elimu hiyo ya udhibiti wa magonjwa, Mkurugenzi wa Utafiti wa TALIRI Dr. Andrew Chota amesema ni wakati mwafaka sasa wafugaji wanapaswa kuzingatia hitaji la kutumia mbinu za kuthibiti vimelea vya magonjwa kuwafikia mifugo (Biosecurity) na kuzingatia ufugaji unaozingatia usalama dhidi ya vimelea hatari vya magonjwa (biosafety)
Aidha, Dr. Chota amewasisitiza wafugaji hao juu ya matumizi ya viosha miguu vyenye dawa na matumizi ya madirisha yenye wavu kuzuia mwingiliano wa wanyama na wanyama wasiotarajiwa.
Kwa upande wake Ndg. Joshua Sina mtaalamu wa malisho wa TALIRI Mpwapwa amewataka wafugaji hao kutenga maeneo ya kupanda malisho kwenye maeneo wanayoyatumia kulishia mifugo ili kuboresha afya za mifugo na hivyo kupata mazao bora ya mifugo ikiwemo nyama, maziwa na ngozi.
Akishukuru baada ya kupata elimu hizo Ndg. Sayuni Miligo mmoja kati ya wafugaji hao amesema elimu waliyoipata itawawezesha wafugaji hao kuweza kuboresha mifugo yao.