BBT PROJECT I KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA 150,000 KWA VIJANA KATIKA BIASHARA ZA KILIMO NA MIFUGO
Serikali kupitia Mpango wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT– Project I) inaendelea kutekeleza mkakati wa kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika biashara za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuongeza ajira, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa. Akitoa wasilisho kuhusu utekelezaji wa mradi huo wakati wa kikao cha uandaaji wa moduli na mwongozo wa unenepeshaji wa mbuzi na kondoo Bw. Tumsime Mutta Mtaalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini Mpango wa Mradi wa ‘BBT Project I’ amesema mpango huo umeanzishwa kufuatia maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha vijana kutumia fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo ili kujiajiri na kuongeza kipato. Bw. Mutta ameeleza kuwa mradi huo unafadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambayo imetoa takribani dola za Marekani milioni 129.71 kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi. Kwa mujibu wa Bw. Mutta, BBT Project I inalenga kuwafundisha na kuwawezesha vijana wapatao 11,000 kupitia programu za uatamiaji na ukuzaji wa biashara za mifugo, huku ikitarajiwa kuanzisha biashara zaidi ya 6,000 zinazomilikiwa na vijana pamoja na kuzalisha ajira za moja kwa moja zipatazo 150,000. Vilevile, Bw. Mutta amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi utahusisha uendelezaji wa mashamba ya pamoja ya kibiashara yenye ukubwa wa takribani ekari 43,500, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, barabara za mashambani, makazi ya vijana, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa zinazokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Bw. Mutta amesema mradi utawezesha vijana kupata mikopo yenye masharti nafuu, kujengewa uwezo wa kuandaa miradi inayovutia uwekezaji, pamoja na kuwaunganisha na wawekezaji na masoko ya uhakika kupitia ushiriki wa sekta binafsi. Mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Dodoma na Mbeya, ukilenga kuwafikia vijana wasiokuwa na ajira pamoja na wale ambao tayari wanajihusisha na biashara za ufugaji lakini wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mitaji ya kukuza shughuli zao.
