Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TEKNOLOJIA YA UHIMILISHAJI YAHITAJI USIMAMIZI BORA ILI KULETA MATOKEO CHANYA
19 May, 2026
TEKNOLOJIA YA UHIMILISHAJI YAHITAJI USIMAMIZI BORA ILI KULETA MATOKEO CHANYA

Wafugaji wengi wamekuwa wakilalamikia teknolojia ya uhimilishaji wakidai kuwa hushindwa kupata matokeo wanayoyatarajia. Hata hivyo, wataalamu wa mifugo wanaeleza kuwa mafanikio ya uhimilishaji hutegemea zaidi usimamizi bora wa mifugo pamoja na maandalizi sahihi kabla ya zoezi hilo kufanyika.

Hali hiyo imedhihirishwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki kupitia Mradi wa Maziwa Faida, ambapo imefanikiwa kupata ndama 60 wanaoendelea kuzaliwa kati ya ng’ombe 80 waliohimilishwa kwa kutumia teknolojia ya uhimilishaji.

Mafanikio hayo yametokana na kuzingatia utaratibu sahihi wa upandishaji wa mifugo kwa mkupuo pamoja na matumizi ya mbegu bora kutoka Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC).

Matokeo hayo yanaonyesha wazi kuwa matumizi sahihi ya teknolojia ya uhimilishaji yanaweza kuongeza ubora wa mifugo, uzalishaji wa maziwa pamoja na tija kwa mfugaji.

Ili kupata matokeo bora ya uhimilishaji, mfugaji anapaswa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha ng’ombe ana afya nzuri na hana magonjwa, kumpatia lishe bora yenye virutubisho vya kutosha, kufuatilia kwa usahihi dalili za joto (heat signs), kuhakikisha ng’ombe amefikia umri na uzito unaofaa kwa kuhimilishwa, kuhakikisha uhimilishaji unafanywa na mtaalamu mwenye ujuzi na kufanya ufuatiliaji baada ya uhimilishaji ili kubaini mafanikio mapema.

Usikose kushiriki Siku ya Maonesho ya Ubunifu na Teknolojia katika Sekta ya Maziwa (TALIRI Open Day 2026 ) itakayofanyika tarehe 11 Juni 2026 katika viwanja vya TALIRI Tanga.

Kupitia maonesho hayo utapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu teknolojia ya uhimilishaji wa mifugo, ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa na mengine mengi kuhusu ufugaji

Karibu sana!

“TALIRI — Utafiti kwa Maziwa Zaidi”

Kumbuka Maziwa Faida ni mradi unaolenga kuboresha mnyororo wa thamani wa ng’ombe wa maziwa unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti, Ushauri na Mafunzo ya Kilimo na Chakula nchini Ireland (Teagasc), kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.