Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
KIFAA MUHIMU CHA KUPIMA UBORA WA MAZIWA
14 Nov, 2024
KIFAA MUHIMU CHA KUPIMA UBORA WA MAZIWA

‘Milk Safe Mini Incubator’ ni kifaa kinachopima ubora wa maziwa kwa kuangalia kama maziwa yana mabaki ya ‘antibiotiki’ hatarishi kwa afya za walaji na kugundua kama kuna uwepo wa sumu kuvu kwenye maziwa ambapo kifaa hicho kinauwezo wa kuona aina tatu za ‘antibiotiki’ zikiwemo ‘beta-lactams, tetracyclines na sulphonamides’ Maziwa yanayoweza kupimwa ni kutoka moja kwa moja kwa ngombe, mbuzi au kondoo, maziwa mabichi, yaliyosindikwa na maziwa ya unga yenye krimu au mafuta.

Hayo yameelezwa na Valentino Urassa Mtafiti Mwandamizi anayesimamia Maabara ya Lishe ya Wanyama iliyopo kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki.

Urassa ameendelea kueleza kuwa lengo kuu la kupima maziwa hayo ni kuhakikisha maziwa yanayozalishwa na wafugaji yanakuwa salama kwa watumiaji kwani upimaji huo unawezesha kujua ukubwa wa tatizo na kutoa ushauri unaostahili kwa wadau wa sekta ya mifugo na kuwaelimisha wafugaji umuhimu wa kufuata kanuni za matumizi ya madawa ya mifugo kwa kufuata maelekezo ya maafisa afya wa mifugo au madaktari wa mifugo.

'Milk Safe Mini Incubator’ ni moja ya vifaa muhimu vinavyopatikana katika maabara hiyo ambapo wafugaji na wadau mbalimbali wa mifugo wanaweza kupeleka sampuli za maziwa kwa ajili ya kupimwa na kifaa hicho. Upatikanaji wa kifaa hicho umewezeshwa na Mradi wa Maziwa Faida wenye lengo la kuongeza mnyororo wa thamani wa maziwa kwa wafugaji unaotekelezwa na kituo hicho uliofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland Nchini Tanzania chini ya Usimamizi wa Dkt. Zabron Nziku ambae ni Mkurugenzi wa kituo hicho.