Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
BALOZI MBAROUK APONGEZWA NA UTAFITI WA TALIRI
12 Aug, 2025
BALOZI MBAROUK APONGEZWA NA UTAFITI WA TALIRI

Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Italia na Mwakilishi wa Kudumu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (FAO, WFP na IFAD) Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa jitihada zake za kubuni na kuibua teknolojia bora za mifugo hususani teknolojia ya jiwe lishe.

Balozi Mbarouk ametoa pongezi hizo leo tarehe 07/08/2025 alipotembelea banda la TALIRI yanapoendelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ‘Nanenane’ viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

“Nimefurahishwa na teknolojia ya jiwe hili kwani ni jiwe tofauti na mawe mengine na nimeambiwa hapa lina viini lishe muhimu kwa mifugo, rai yangu kwa taasisi hii ni kuzalisha jiwe hili kwa wingi na kulisambaza kwa wafugaji ili kuongeza tija ya ufugaji” alisema Balozi Mbarouk.

Akielelezea jiwe hilo Bw. Ezekiel Maro Mtafiti wa Taasisi hiyo amesema jiwe hilo ni tofauti na mawe mengine kwa kuwa lina viini lishe muhimu kwa mnyama kwa ajili ya kumuwezesha kupata wanga, protini pamoja na madini.

Maro ameongeza kuwa jiwe hilo linafaa kutumiwa na wanyama wote wenye uwezo wa kulamba na kutafuna, lina ladha inayovutia pia linasambazwa kwa gharama nafuu ukilinganisha na yale ya viwandani.

“TALIRI imezalisha jiwe hilo kwa lengo la kumuwezesha mfugaji kutumia jiwe moja lenye viini lishe vya madini, protini na wanga vinavyofaa kwa mnyama kwa wakati mmoja badala ya kutumia mawe yenye viini lishe vya aina moja pekee” aliongeza Maro.