Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
FAHAMU AINA YA NG'OMBE ANAYEFANYA VIZURI NYANDA KAME
21 May, 2024
FAHAMU AINA YA NG'OMBE ANAYEFANYA VIZURI NYANDA KAME

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kupitia kituo cha TALIRI Mpwapwa imefanya utafiti na kuzalisha mbari ya ng’ombe aina ya Mpwapwa kwa lengo la kuongeza lishe na kipato kwa wananchi wa mikoa ya nyanda kame.

Utafiti huu wa kuzalisha ng’ombe aina ya Mpwapwa ulifanyika miaka ya 1960 kutokana na changamoto walipitia wafugaji wa mikoa ya nyanda kame, ikiwemo uzalishaji mdogo wa maziwa ambapo walikuwa wanapata lita moja na nusu hadi tatu kwa siku kwa ng’ombe mmoja na kiasi kidogo cha nyama.

Ng’ombe aina ya Mpwapwa ni mchanganyiko wa damu ya ng’ombe kutoka mabara ya Ulaya, Asia, Afrika, na ng’ombe wa asili wa hapa nchini. Ng’ombe huyu amezalishwa kuwa na uwezo wa kuhimili mazingira ya ukame yenye uhaba wa malisho na maji, bila kuathiri utoaji wa maziwa na nyama. Pia, wana uwezo wa kustahimili baadhi ya magonjwa.

Jike anaweza kupandishwa akiwa na umri wa kati ya mwaka mmoja na nusu hadi miwili, ukilinganisha na miaka mitatu kwa ng’ombe wa asili. Ng’ombe huyu akifugwa kwenye kanda kame ana uwezo wa kutoa maziwa lita 6 hadi 8 kutegemea na matunzo ya mfugaji, hii ni mara tatu zaidi ya maziwa anayotoa ng’ombe wa asili wa Tanzania aina ya zebu.

Sambamba na sifa hizo, ng’ombe aina ya Mpwapwa ana umbile kubwa ukilinganisha na ng’ombe wa asili, ambapo dume ana uwezo wa kutoa nyama kiasi cha kilo 230 akiwa na umri wa miaka minne.

Wafugaji wa mikoa ya kanda ya kati yaani nyanda kame ukiwemo mkoa wa Dodoma na Singida mnakaribishwa kutembelea kituo cha TALIRI Mpwapwa na TALIRI Kongwa kwa ajili ya kujifunza zaidi juu ya ufugaji wenye tija.