VITU VYA KUZINGATIA NDAMA ANAPOZALIWA

Ubora wa ng’ombe unatokana na matunzo bora aliyopatiwa tangu alipozaliwa yaani umri wa ndama, endapo mfugaji atazingatia kumpa ndama matunzo bora basi ni wazi kuwa uzalishaji wa mifugo yake utaimarika na hivyo kumuwezesha kuwa na ufugaji wenye tija.
Mara baada ya ndama kuzaliwa hakikisha anapata maziwa ya kwanza ya ng’ombe yaani Dang’aa ‘Colostrum’ Dang’aa ni maziwa ya kwanza kutoka kwenye chuchu za ng’ombe ambayo ndama anapaswa kupatiwa ndani ya masaa 24 mara baada ya kuzaa na ndio chanzo cha kwanza cha virutubisho kwa ndama.
Maziwa hayo ya kwanza yana virutubisho vingi ambavyo ni muhimu katika ukuaji wa ndama vikiwemo vitamini na madini, pia humpatia ndama kinga dhidi ya magonjwa, na inashauriwa mfugaji kuhakikisha ndama amekunywa maziwa hayo ya mwanzo ya kutosha kwa kumpatia ndama mara nyingi kiasi kidogo kidogo kabla ya siku hiyo ya kuzaliwa kuisha.
Ndama atenganishwe na mama yake ndani ya masaa mawili mara baada ya kuzaliwa, akae chumba cha peke yake na aendelee kunyweshwa maziwa ya kwanza ya mama kwa siku 3 hadi 5 na baada ya hapo ndama anaweza kuchanganywa na ndama wengine na kunywa maziwa mchanganyiko toka kwa ng’ombe wengine.
Lakini pia ndama awekewe alama ya utambulisho (hereni) sikioni ndani ya siku moja mara baada ya kuzaliwa na apakwe ayodini (dawa) kwenye kitovu ili kuzuia maambukizi pia apatiwe chanjo muhimu inapobidi.
Ndama apimwe uzito (kilogramu) ndani ya masaa 12 baada ya kuzaliwa na apelekwe kwenye chumba anachoweza kukaa peke yake huku akiendelea kupimwa uzito wake kila wiki ili kujua maendeleo yake ya makuaji.
Tambua kuwa maandalizi ya ndama anapozaliwa yanaanzia kwa ngómbe anayetaka kuzaa, ni lazima kumtambua ng’ombe anayekaribia kuzaa na kumuweka eneo maalumu lililotengwa na kuandaliwa kwa ajili ya ng’ombe kuzalia ambalo linaweza kuwa ndani ya banda lenye nafasi kubwa lakini inapendekezwa eneo liwe la uwazi mpana na kuwekewa majani makavu.