Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MWENYEKITI WA BODI YA TIC AFURAHISHWA NA ELIMU YA UHIMILISHAJI WA KUKU TALIRI
09 Aug, 2024
MWENYEKITI WA BODI YA TIC AFURAHISHWA NA ELIMU YA UHIMILISHAJI WA KUKU TALIRI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dkt. Binilith Mahenge amefurahishwa na elimu ya uhimilishaji wa kuku mara bak namna kitendo hicho cha uhimilishaji wa kuku kwa njia rahisi kinavyofanyika.

Dkt. Mahenge ameeleza kufurahishwa huko alipotembelea banda la TALIRI kwa lengo la kupata elimu juu ya teknolojia bora za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo katika Maonesho ya 31 ya Kilimo ya Kimataifa (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika Kanda ya Kati ndani ya viwanja vya Nzuguni Dodoma yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’

“Hii ni teknolijia muhimu sana kwa wafugaji wa kuku kuijua kwani inafanyika kwa urahisi kiasi cha kumuwezesha mfugaji wa hali yoyote kumudu kuifanya” alisema Dkt. Mahenge.

Sambamba na hayo Dkt. Mahenge amepata fursa ya kupata elimu ya mbari bora za mifugo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na mazao mengine ya mifugo ikiwemo na elimu ya mbegu bora za malisho na vyakula vya mifugo kutoka kwa wataalamu wa taasisi hiyo.

Akielezea faida za uhimilishaji wa kuku Mtafiti wa taasisi hiyo Ndg. Jefta Mgalula amesema kwa mkamuo mmoja wa mbegu za jogoo unaweza kupandisha kati ya matetea sita hadi nane wakati ukimruhusu jogoo kumpanda tetea kwa njia ya kawaida mbegu hizo zitabaki kwa tetea mmoja.

Pamoja na hayo kwa kutumia teknolijia ya uhimilishaji mfugaji anaweza kuchukua mbegu za jogoo bora mwenye umri mkubwa au aliyevunjika mguu na kukosa uwezo wa kumpanda tetea, sambamba na hayo kupitia uhimilishaji mfugaji anaweza kutumia kutumia mbegu za jogoo mkubwa ama mdogo na kuziweka kwa tetea pia kitendo cha uhimilishaji kinamsaidia tetea kupunguza maumivu kutokana na kitendo cha kupandwa na jogoo.

Uhimilishaji wa kuku ni kitendo cha kuvuna mbegu za jogoo na kuziweka kwenye njia ya uzazi wa tetea.

Mara nyingi kitendo hiki hufanyika kwa jogoo aina ya kuchi kwani kuku huyo ameonekana kupendwa zaidi na wafugaji kwa sababu ana thamani kubwa lakini pia uzalianaji wake ni mdogo kutokana na tabia ya kuku huyo kupenda kupigana muda mwingi na kupelekea kuzaliana kwake kuwa ni kwa kiwango kidogo hata tetea wake wana uwezo mdogo wa kuangua mayai