Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
UBALOZI WA IRELAND NCHINI TANZANIA WAFURAHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI, TALIRI
01 Nov, 2024
UBALOZI WA IRELAND NCHINI TANZANIA WAFURAHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI, TALIRI

Viongozi wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania wakiongozwa na Naibu Mkuu wa Ushirikiano Hellen Counihan wamefurashwa na namna Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) inavyosimamia vyema utekelezaji wa mradi wa Maziwa Faida unaofadhiliwa na Ubalozi huo.

Viongozi hao wameeleza kufurahishwa huko leo tarehe 23/10/2024 walipotembelea kituo cha taasisi hiyo cha TALIRI Kanda ya Mashariki kinachotekeleza mradi huo kwa lengo la kujionea namna ambavyo kituo hicho kinatekeleza mradi huo.

Akiongea Hellen amesema amefurahishwa namna ambavyo shughuli za utekelezaji wa mradi huo zinazingatia malengo mahususi ya mradi hususani kuongeza mnyororo wa thamani wa maziwa kwa wafugaji.

“Nimekulia kwenye jamii ya wafugaji lakini sikuwa najua mambo mengi juu ya ufugaji kama ambavyo nimejionea na kujifunza hapa leo mnafanya kazi nzuri sana hongereni” aliongeza Hellen 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku ameeleza kupitia mradi wa maziwa faida uzalishaji wa malisho umeongezeka kutoka kuzalisha marobota 300 hadi 4,000 kwa mwaka 2023/2024, kuzungushia uzio mashamba ya malisho, maonyesho ya mfumo wa kilimo bora kwa kuanzisha shamba darasa  ‘satellite farms’ na uzalishaji bora wa malisho huko Muheza na kufanikiwa kupendekeza aina ya malisho bora kwa ukanda wa Pwani.

Sambamba na hayo Dkt. Nziku ameeleza kuwa mradi umewezesha kusomesha ngazi ya shahada ya uzamili wataalamu 8, kuboresha maabara ya lishe ya wanyama, kufanya ukarabati wa baadhi ya miundombinu ya taasisi na ununuzi wa vitendea kazi.
 
Mradi wa maziwa faida umelenga kusaidia mageuzi jumuishi yenye ushindani endelevu na yanayostahimili hali ya hewa na mnyororo wa thamani wa ng'ombe wa maziwa nchini, unaotokana na uboreshaji wa uwezo miongoni mwa wahusika katika msururu huo na kuimarishwa kwa uwezo wa kitaasisi ili kutoa ubunifu unaoongozwa na utafiti.

Akiongea kwa niaba ya wafugaji wengine Edna Nkya amesema kupitia mradi huo ameweza kujifunza aina na kiasi cha chakula ambacho ng’ombe anapaswa kula kwa siku kitendo ambacho kimepelekea kuongezeka kwa maziwa kumuwezesha kumudu gharama za maisha na hivyo kuweza kusomesha wanawe kwenye Shule nzuri kutokana faida anayoipata kwa sasa baada ya kuuza maziwa.

Mradi wa Maziwa Faida kwa sasa unatekelezwa Mkoani Tanga pekee huku malengo yakiwa ni kuwezesha mradi kufikia wafugaji wote nchini.