Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MAJANI MAKAVU KUWEZESHA LISHE TOSHELEVU
19 Jul, 2024
MAJANI MAKAVU KUWEZESHA LISHE TOSHELEVU

Wafugaji wameendelea kupatiwa elimu ya lishe kwa wanyama ambapo wameshauriwa kuwapatia wanyama kama ng’ombe majani makavu yaliyokauka kwa wastani wa asilimia 80 - 100 ya ukavu ili kuwawezesha kupata lishe inayotosheleza kuzalisha nyama au maziwa kwa wingi kulingana na uwezo wa ‘kijenetiki’ wa mnyama husika.

Elimu hiyo imetolewa leo tarehe 04/07/2024 na Bw. Ezekiel Maro Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wakati akimuelezea mdau aliyetembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kupata elimu juu ya teknolojia mbalimbali za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es salaam yakiwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania: Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji”

Maro ameendelea kueleza kuwa mifugo inatakiwa kula majani makavu sababu anapokula majani mabichi hulazimika kula mengi na kwakuwa majani hayo huwa na maji mengi hupelekea mnyama kupata lishe ndogo.

“Kimsingi majani mabichi kuchukua nafasi kubwa tumboni na kumpelekea mifugo kushindwa kula vizuri vyakula vingine vya kumuongezea lishe mwilini ikiwa atapatiwa vyakula hivyo baada ya kula majani mabichi” aliongeza Maro.

Aidha, Maro ameeleza kuwa inashauriwa mnyama kupewa jiwe la kulamba la madini ili kumrejeshea virutubisho vilivyopotea baada kukauka kwa majani.

Ewe mfugaji tembelea vituo vya TALIRI vinavyopatikana katika kanda saba nchini ikiwemo kanda ya kati, kanda ya mashariki, kanda ya kusini, kanda ya kaskazini, kanda ya nyanda za juu kusini, kanda ya Magharibi na Kanda ya Ziwa ili uweze kupata elimu juu teknolojia za mifugo zilizoibuliwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuwezesha kuongezeka kwa mnyororo wa thamani wa mifugo.