Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
NAIBU KATIBU MKUU MIFUGO AITAKA TALIRI NA ILRI KUENDELEA KUFANYA TAFITI ZA MIFUGO
01 Nov, 2024
NAIBU KATIBU MKUU MIFUGO AITAKA TALIRI NA ILRI KUENDELEA KUFANYA TAFITI ZA MIFUGO

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Ndg. Abdul Mhinte ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI)  na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI ) kuendelea kufanya utafiti ili kuwezesha kupatikana kwa ng’ombe bora zaidi wa maziwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi na hivyo kuwanufaisha zaidi wafugaji na kukuza mchango wa tasnia ya maziwa katika uchumi wa Taifa.

Mhinte ametoa wito huo leo tarehe 31/10/2024 katika mafunzo ya uzinduzi wa Mfumo wa Kidijitali wa kukusanya takwimu uitwao ‘AADGG-Diary Data App’ kwa maafisa ugani wanaochukua takwimu za kuboresha mbari za ng’ombe wa maziwa kupitia mradi wa ‘African Asia Diary Genetic Gain (AADGG)’ unaotekelezwa na TALIRI kwa kushirikiana na ILRI yaliyofanyika ukumbi wa African Dreams Hotel Mkoani Dodoma.

Sambamba na hayo Mhinte ameeleza kuwa Wizara hiyo imenufaika na mradi wa AADGG kwa kuona umuhimu wa kutoa huduma za ugani kwa kutumia mtandao wa kidigitali na pia kuwatembelea wafugaji angalau mara moja kila mwezi na kwamba Wizara itaendelea kujifunza mengine mengi mazuri kupitia utekelezaji wa mradi huo kwa nia ya kuwezesha ukuaji wa sekta za Mifugo na Uvuvi.

Aidha, Mhinte ametoa shukrani kwa ILRI kwa kushirikiana na TALIRI na wadau wengine kwa kuchagua kutekeleza mradi huo hapa nchini ikiwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo kunufaika na mradi huo ambao ulianza tangu mwaka 2016 na amezitaka taasisi hizo kuwezesha mradi huo kuwafikia wafugaji wote wa ng’ombe wa maziwa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba amesema mradi wa AADGG ulianzishwa kwa madhumuni ya kuanzisha kanzidata kwa ajili ya kupokea na kuchakata taarifa za uzalishaji ng’ombe wa maziwa nchini, kutambua, kuthibitisha na kuhamasisha matumizi ya ng’ombe bora wa maziwa mwenye kustahimili mazingira mbalimbali nchini na kuanzisha jukwaa la kidigitali la kukusanya taarifa za uzalishaji na kutoa mrejesho wa namna bora ya kutunza na kuboresha ng’ombe wa maziwa.

Prof. Komba ameendelea kueleza kuwa kwa sasa mradi huo unatekelezwa katika mikoa saba ukiwemo Mkoa wa Mbeya, Njombe, Songwe, Iringa, Tanga, Kilimanjaro na Arusha ikiwa na jumla ya Halmashauri 24 zinazotekeleza mradi huo na ambayo Maafisa Ugavi wake wanapatiwa mafunzo hayo leo lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi wa ukusanyaji takwimu za mradi huo kwa maslahi ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Nae Dkt. Eliamoni Titus Lyatuu Mratibu wa Mradi wa AADGG Kitaifa amesema miongoni mwa taarifa zinazokusanywa ni pamoja na taarifa za usajili wa mfugaji, ng’ombe, vyama vya ushirika/makundi ya wafugaji, taarifa za maendeleo ya mifugo kama uchochezi wa mimba, uzao, maziwa, afya ya mifugo, uzito, taarifa za manyoya ya ng’ombe kwa ajili ya kupima vinasaba vya ng’ombe na taarifa za kaya ya mfugaji.

Pamoja na hayo Dkt. Lyatuu ameeleza kuwa taarifa za takwimu hizo baada ya kukusanywa, TALIRI, ILRI na Viongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi watakuwa na uwezo wa kuona takwimu hizo.