Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
BODI YA WAKURUGENZI YA TALIRI YAKAGUA UJENZI WA OFISI ZA TAASISI SITA ZA SEKTA YA MIFUGO
28 Sep, 2026
BODI YA WAKURUGENZI YA TALIRI YAKAGUA UJENZI WA OFISI ZA TAASISI SITA ZA SEKTA YA MIFUGO

Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Esron Karimuribo, imekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Ofisi za Taasisi sita zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Sekta ya Mifugo.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Wakala ya Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA), Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) pamoja na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Prof. Karimuribo amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Kampuni ya Ujenzi ya China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Co. Ltd. (CJIETC), kuhakikisha ujenzi unakamilika ndani ya muda uliopangwa na kwa kuzingatia viwango na ubora unaohitajika.

Aidha, Prof. Karimuribo ameitaka TALIRI kuendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, kwa kuzingatia matakwa ya mkataba na viwango vilivyowekwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, amesema Taasisi itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unatekelezwa kwa tija na kukamilika kwa wakati.

Prof. Komba amesema kuwa kwa mujibu wa mkataba, mradi huo umegharimu jumla ya Shilingi bilioni 54.5 ikijumlisha Mkataba wa Mkandarasi na Mshauri Mwelekezi wa Mradi, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2027.

Nae Msimamizi wa Mradi Mhandisi Edwinbright Masawe kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), amesema kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia mbili (2%).

Mhandisi Masawe amesema kuwa TBA itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo kuhakikisha Mkandarasi anazingatia ratiba ya ujenzi, viwango vya ubora na matakwa ya mkataba, ili mradi ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.