PROF. KARIMURIBO AITAKA TALIRI KUHAKIKISHA MRADI WA BBT PROJECT I KUTEKELEZWA KWA UBORA
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Esron Karimuribo, ameitaka Taasisi hiyo kuhakikisha inatekeleza kwa ufanisi Mradi wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT) Project I unaotekelezwa katika Kituo cha TALIRI Kongwa, Dodoma.
Prof. Karimuribo ametoa agizo hilo leo, Septemba 10, 2026, alipofanya ziara katika Kituo cha TALIRI Kongwa kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Mradi huo. Katika ziara hiyo aliambatana na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TALIRI.
Prof. Karimuribo amesema TALIRI ina nafasi muhimu katika kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi yanafikiwa, hususani kupitia tafiti, teknolojia na utaalamu wa kitaalamu unaotolewa na Taasisi hiyo.
“Ninatamani kuona TALIRI inashiriki kikamilifu kwa kutoa utaalamu katika kuwezesha utekelezaji wa Mradi huu kwa ufanisi, ili vijana wanaonufaika waweze kupata maarifa, ujuzi na mazingira bora ya kufanya shughuli za uzalishaji na biashara za mifugo,” amesema Prof. Karimuribo.
Akielezea namna Mradi huo utakavyotekelezwa, Mratibu wa Mradi wa BBT Project I – Mifugo, Bw. Daud Mayeji, amesema Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambapo Kituo cha TALIRI Kongwa ni eneo la utekelezaji.
Bw. Mayeji amesema Mradi umelenga kuwawezesha zaidi ya vijana 14,000 kupitia programu za uatamiaji na ukuzaji wa biashara za mifugo, huku ukitarajiwa kuchochea uanzishwaji wa ajira zaidi ya 10,000.
Ameeleza kuwa miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya Kituo cha TALIRI Kongwa, uendelezaji wa mashamba, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na ujenzi wa makazi kwa ajili ya vijana watakaonufaika na Mradi huo.
Aidha, amesema Mradi utawawezesha vijana kupata mikopo yenye masharti nafuu, kujengewa uwezo wa kuandaa na kuendesha miradi ya biashara, pamoja na kuwaunganisha na wawekezaji na masoko ya uhakika kupitia ushiriki wa Sekta binafsi.
