Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
Wasifu
Sebastian Wilson Chenyambuga photo
Prof. Sebastian Wilson Chenyambuga
Mwenyekiti wa Bodi

: hq@taliri.go.tz

: +255 026 - 296 1954

Wasifu wa Prof. Sebastian Wilson Chenyambuga

Sebastian Wilson Chenyambuga alizaliwa tarehe 15 Aprili 1965 katika kijiji cha Salama, wilaya ya Magu, Tanzania. Alisoma elimu ya shule ya msingi katika shule ya msingi Nyankonya, wilaya ya Magu kuanzia 1974 hadi 1980, elimu ya sekondari ya kawaida (O'leve) katika shule ya sekondari Mpwapwa, wilaya ya Mpwapwa kuanzia 1981 hadi 1984 na elimu ya sekondari ya Juu (A' level) katika shule ya sekondari ya Kibaha kuanzia mwaka 1985 hadi 1987. Alisoma Shahada Sayansi katika Kilimo (chaguo la sayansi ya wanyama) kutoka 1989 hadi 1991, Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Kilimo (Uzalishaji wa Wanyama) mwaka 1992 hadi 1994 na Shahada ya Uzamivu katika Mbari za Wanyama (PhD Animal Genetics) kuanzia 1997 hadi 2002 katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Tanzania. Wakati wa masomo yake ya shahada ya Uzamivu, alihudhuria mafunzo ya uchanganuzi wa mbari za wanyama katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Wageningen, Uholanzi. Alifanya kazi yake ya utafiti wakati wa shahada ya uzamivu katika Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Nairobi, Kenya (1998 na 2000), na Chuo Kikuu cha Liverpool, Uingereza (1999). Utafiti wake wa shahada ya uzamivu ulikuwa juu ya anuwai ya mbari za mbuzi wa kienyeji wa Afrika waliopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Amehudhuria kozi fupi za usimamizi Bora wa Shahada za Uzamivu (2009) na  ufundishaji na mbinu za kujifunza kwa kutumia majaribio ya kisayansi (2014) katika idara ya Elimu ya Sayansi, Chuo Kikuu cha Copenhagen.

Prof. Chenyambuga aliajiriwa Desemba 1991 na Wizara ya Kilimo kama Afisa Utafiti wa Mifugo katika Taasisi ya Utafiti wa Uzalishaji Mifugo, Mpwapwa, Tanzania. Mwaka 1995 aliajiriwa kama Mtafiti Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine . Aliajiriwa kama Mhadhiri Msaidizi mwaka 2000 katika Idara ya Sayansi ya Wanyama na Uzalishaji, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine . Alipandishwa cheo kutoka Mhadhiri Msaidizi hadi Mhadhiri mwaka 2003, Mhadhiri Mwandamizi mwaka 2006, Profesa Mshiriki mwaka 2010 na Profesa Kamili mwaka 2015. Prof Chenyambuga anafanya kazi ya uprofesa katika Idara ya Wanyama, Ufugaji wa Samaki na Sayansi ya Nyanda za Malisho, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.

Pia aliwahi kuteuliwa kuwa Naibu Amidi-Utawala katika Kitivo cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (2014 - 2017). Aliteuliwa kuwa Mkuu wa idara, Idara ya Wanyama, Ufugaji wa Samaki na Sayansi ya Nyanda za malisho, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (2019 - 2022). Aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Nyama Tanzania (2015 – 2018). Aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) (2019 – 2022). Kwa sasa ameteuliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa awamu ya pili (2022 – 2025)

Prof Chenyambuga anafundisha kozi zinazohusiana na mbari za wanyama na bioteknolojia ya wanyama kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza na masomo ya uzamili. Pia, anafundisha kozi za mbinu za utafiti. Amesimamia wanafunzi 27 wa shahada ya Uzamili na wanafunzi 7 wa shahada  ya uzamivu . Prof. Chenyambuga amehusika katika miradi 22 ya utafiti na aliwahi kuwa kiongozi wa mradi kwa miradi 10. Kazi yake ya utafiti imekuwa zaidi katika ng'ombe, mbuzi na sato wa mto Nile, haswa katika taaluma za mbari za wanyama na lishe ya wanyama. Amechapisha machapisho ya kisayansi 57 katika majarida yanayotambulika kimataifa na  machapisho 38 yaliyowalishwa katika shughuli za mkutano.