TALIRI YAENDESHA MAFUNZO KWA WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Esron Karimuribo, amesema wajumbe wa Bodi wana wajibu wa kuhakikisha wanasimamia rasilimali za taasisi kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa utendaji kazi wa watumishi wa Taasisi ili kuimarisha Sekta ya Mifugo kwa maslahi ya Taifa.
Prof. Karimuribo ameyasema hayo leo, Septemba 11, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Wajibu na Majukumu ya wajumbe wa Bodi katika kusimamima taasisi na mashirika ya Umma na masuala ya uendelevu wa mazingira, jamii na Utawala Bora (ESG), kwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TALIRI yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, jijini Dodoma.
Prof. Karimuribo ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia Wajumbe wa Bodi kufahamu kwa kina wajibu wao, mgawanyo wa majukumu na misingi ya usimamizi bora wa taasisi, ili kuhakikisha malengo ya TALIRI yanafikiwa kwa wakati na kwa ufanisi, huku wakizingatia masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Usimamamizi wa Rasilimaliwatu na Mashirika ya Umma kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Hussein Kakurwa amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina ina wajibu wa kusimamia misingi ya uwajibikaji wa bodi zote zinazoteuliwa na Serikali, ili kuhakikisha zinatimiza dhamana waliyopewa katika kusimamia taasisi na mashirika ya Umma.
Nae, Mkaguzi wa Hesabu kutoka Uongozi Institute, FCPA Dkt. Neema Kiure, amewajengea uwezo wajumbe wa Bodi kuhusu namna taasisi zinavyoweza kuchangia katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya 2050 kwa kuzingatia masuala uendelevu wa mazingira, jamii na Utawala Bora (ESG).
Dkt. Kiure amesisitiza umuhimu wa taasisi kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira, kupunguza uchafuzi na hewa ukaa (emissions),katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akihitimisha mafunzo hayo, mmoja wa wajumbe wa Bodi amepongeza uongozi wa TALIRI,kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yamekuwa na manufaa makubwa katika kuwajengea uwezo wajumbe hao na kuahidi kushirikiana kwa karibu na Menejimenti ya TALIRI ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
