Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TFRA,TALIRI KUTEKELEZA MPANGO WA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO
13 Feb, 2026
TFRA,TALIRI KUTEKELEZA MPANGO WA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO

Uelewa mdogo wa wazalishaji wa malisho ya mifugo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea umepelekea kupatikana kwa kiasi kidogo cha malisho ya mifugo kwa wafugaji.

Kutokana na changamoto hiyo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imeandaa Mpango wa Utoaji wa Elimu ya Matumizi Sahihi ya Mbolea katika Uzalishaji wa Malisho ya Mifugo lengo ikiwa ni kuelimisha wafugaji na wazalishaji wa malisho juu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa ajili ya kuongeza tija ya uzalishaji na ubora wa lishe ya mifugo.

Akiongea wakati wa kikao kilichofanyika TALIRI cha kujadili namna mpango huo utatekelezwa  Bi Happiness Mbele Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa TFRA amesema utekelezaji wa mpango huo utahusisha hatua zifuatazo ikiwemo; kuainisha mbolea zinazotumika katika uzalishaji wa malisho, kuainisha mahitaji ya wafugaji na wazalishaji wa malisho, kuanzishwa kwa mashamba darasa ya malisho, kutoa mafunzo kwa wafugaji na wazalishaji wa malisho pamoja na kutoa elimu kwa kutumia vyombo vya habari.

Bi Happiness ameendelea kueleza kuwa kutekelezwa kwa mpango huo kutawezesha kuongezeka kwa tija ya uzalishaji wa malisho, ubora wa lishe ya malisho, kupungua kwa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, kuimarika kwa ushirikiano baina ya TFRA na TALIRI pamoja na utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba amesema moja kati ya majukumu ya Taasisi ni kuhakikisha malisho na mbegu bora za malisho zinapatikana ili kuwezesha ufugaji wenye tija nchini hivyo utekelezwaji wa mpango huo ni hatua muhimu ya kuongeza uzalishaji wa malisho ya mifugo pamoja na mazao ya kilimo.

“Kwa uelewa sahihi wa matumizi ya mbolea, wakulima na wafugaji wana uhakika ya kupata malisho bora na kuongeza uzalishaji wa mifugo kwa tija na faida zaidi” ameongeza Prof. Komba.

TFRA na TALIRI watachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha tija ya uzalishaji wa malisho na mifugo nchini Tanzania kupitia matumizi sahihi ya mbolea, utafiti wa kisayansi, na kueneza teknolojia bora kwa wakulima na wafugaji. Ushirikiano huu ni muhimu kwa kukuza ufugaji endelevu.