Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
WAFUGAJI WA KUKU WASHARIWA KUSUBIRI CHANJO KUISHA KABLA YA KUTUMIA MAZAO YAKE
13 Feb, 2026
WAFUGAJI WA KUKU WASHARIWA KUSUBIRI CHANJO KUISHA KABLA YA KUTUMIA MAZAO YAKE

WAFUGAJI WA KUKU WASHAURIWA KUSUBIRI CHANJO KUISHA KABLA YA KULA MAZAO YAKE: Wafugaji wa kuku wameshauriwa kusubiri siku 3 hadi 8 baada ya kuchanja kabla ya kula mayai au nyama ya kuku ili kuipa muda dawa kuisha mwilini mwa mnyama na hivyo kuboresha afya ya mlaji.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Utafiti kutoka TALIRI Makao Makuu Dkt. Andrew Chota wakati wa mafunzo ya ufugaji wa kuku kisasa kwa wafugaji walioko wilaya ya Kongwa na maeneo ya karibu yaliondeshwa kupitia kituo chake cha Kanda ya Kati cha Kongwa yaliyofanyika tarehe 28/ 01/ 2025 katika ukumbi wa mkutano uliopo kituoni hapo.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wafugaji wa kuku kwa njia za kisasa, ambapo wamepewa elimu juu ya sifa na ujenzi wa mabanda bora ya kuku, utunzaji bora wa vifaranga, lishe ya kuku na namna ya kuchanganya vyakula, magonjwa hatarishi ya kuku na aina za chanjo na udhibiti wa vimelea vya magonjwa bandani na mbinu za kufikia masoko.

Dkt Chota amewataka wafugaji kufuata ushauri wa kitaalamu kwa kuzingatia ufugaji unaolingana na ukubwa wa eneo kwa idadi stahili ya kuku, mzunguko bora wa hewa bandani, mwanga na mwelekeo wa jua. Pia ameendelea kueleza kuwa wafugaji wanatakiwa kuzingatia matumizi ya vyombo vya kulishia na kunyweshea kuku kwa idadi ya kuku 25 kwa chombo kimoja ili kupunguza changamoto za magonjwa na uzalishaji duni. 

Akielezea magonjwa yanayoambukiza Dkt. Edwin Mtei ambae ni Daktari wa mifugo kituoni hapo ameeleza kuwa magonjwa hayo husambazwa kwa bakteria na virusi ambao husabaisha magonjwa kama homa ya matumbo, mdondo, kipindupindu cha kuku na ndui.

Sambamba na hayo Dkt. Mtei ameeleza kuwa magonjwa haya yanadhibitiwa kwa njia mbalimbali kama vile kuchanja, kuzingatia usafi wa chakula, na udhibiti wa vimelea vya magonjwa kuingia bandani kwa kutengeneza kiosha miguu na kuweka dawa (footbath) kabla ya kuingia bandani.

Akishukuru baada ya mafunzo hayo, Bi Zuhra Bosco ambaye ni mfugaji wa kuku wa mayai na wa nyama ameiomba TALIRI kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara na kwa wafugaji wengi zaidi ili kuwezesha ufugaji wenye tija.